
COP30 inafanyika baada ya miaka miwili mfululizo yenye rekodi ya viwango vya juu zaidi vya joto duniani na kuendelea kwa ongezeko la gesi chafuzi. Wakati huo huo, uhusiano wa kimataifa ambao ni muhimu kwa diplomasia ya tabianchi umekuwa ukitikiswa na vita, migogoro ya kibiashara, na mitazamo tofauti kuhusu mustakabali wa mfumo wa nishati duniani.
“Huu unaweza kuwa mmoja wa mikutano muhimu zaidi ya tabianchi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, lakini hakuna shaka, tunakabiliwa na vikwazo vikubwa.” amesema Ruth Do Coutto, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Mabadiliko ya Tabianchi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP).
Kuanzia kupunguza utoaji wa gesi chafuzi, kulinda misitu, hadi kuimarisha fedha za kukabiliana na athari za tabianchi na mifumo ya tahadhari ya mapema, haya ndiyo masuala sita makuu ambayo wajumbe wanatarajiwa kujadili huko Belém.
1. Jinsi ya kuzuia kuongezeka kwa joto kupita kiasi
Licha ya hatua fulani kufikiwa, mipango ya kitaifa ya hali ya hewa bado ipo mbali sana na kiwango kinachohitajika kuzuia athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti ya UNEP kuhusu Pengo la Uzalishaji 2025, iliyotolewa kabla ya COP30, inaonesha kuwa ahadi za sasa zinaweka dunia kwenye njia ya kuongezeka kwa joto la kati ya nyuzi 2.3–2.5°C kufikia mwisho wa karne hii.
Inawezekana sana kwamba kikomo cha 1.5°C kitazidishwa ndani ya muongo mmoja ujao kipaumbele sasa ni kuhakikisha ongezeko hilo ni dogo na la muda mfupi iwezekanavyo.
2. Jinsi ya kulinda jamii dhidi ya madhara ya tabianchi
Kama ilivyokuwa katika mikutano iliyopita ya COP, mkutano wa Belém utaangazia jinsi nchi zinavyoweza kujiandaa kwa majanga ya hali ya hewa na kuongezeka kwa kina cha bahari.
Nchi zinazoendelea zitahitaji zaidi ya dola bilioni 310 kila mwaka kufikia 2035, lakini kwa sasa zinapata fedha chache mno. Kuwekeza katika utayari kunaleta faida kubwa, kwani kila dola moja inaweza kuokoa hadi dola 15. Kwa kuwa ahadi ya Glasgow inaisha mwaka huu, COP30 inatarajiwa kuweka lengo jipya la kimataifa la fedha za uhimilivu na mfumo wa kufuatilia utekelezaji wake.
3. Jinsi ya kutimiza ahadi ya dola trilioni moja
Kabla ya kuanza kwa COP30, Azerbaijan (mwenyeji wa COP29) na Brazil waliwasilisha mwelekeo wa njia ya kufanikisha dola trilioni 1.3 kwa mwaka kwa ajili ya ufadhili wa hali ya hewa kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2035.
Fedha za umma ni chache, hivyo ni lazima zitumike kuvutia mitaji binafsi kwa kiwango kikubwa kwa miradi ya kupunguza na kukabiliana na madhara ya tabianchi katika nchi zinazoendelea.
Nchi zilizoendelea zinapaswa kuongoza kupitia maboresho ya benki za maendeleo ya kimataifa, suluhisho za deni na mbinu zinazovutia uwekezaji binafsi ili kubadilisha ahadi kuwa vitendo halisi vya kifedha.
4. Jinsi ya kutumia majawabu bunifu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
COP30 itazindua na kuimarisha juhudi bunifu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Miongoni mwao ni kampeni ya Beat the Heat, inayoongozwa na Brazil na UNEP, kusaidia suluhisho za mitaa dhidi ya joto kali na kukuza teknolojia za ubaridi endelevu kama paa baridi na maeneo ya kijani. Pia kuna mradi wa Bairro do Mutirão unaoonesha jinsi miundombinu bunifu inavyoweza kupunguza joto na kuhifadhi rasilimali.
UNEP kwa kushirikiana na wadau itazindua mpango wa Food Waste Breakthrough wa miaka mitano wa kupunguza taka za chakula kwa asilimia 50, kupunguza hadi asilimia 7 ya utoaji wa methane duniani. Aidha, Tropical Forest Forever Facility italipa nchi kulinda misitu ya kitropiki kupitia mfumo wa fedha mchanganyiko. Uzinduzi huu unaunga mkono lengo la COP30 la kujenga dunia endelevu na yenye ustahimilivu zaidi.
5. Jinsi ya kuhakikisha mabadiliko ya haki na jumuishi
Faida za kiuchumi za hatua za hali ya hewa zimekuwa wazi zaidi kuliko hapo awali. Nishati mbadala asa ndiyo chanzo cha umeme cha gharama nafuu zaidi duniani, hutoa ajira, ukuaji wa uchumi na afya bora, huku ikilinda nchi dhidi ya mabadiliko ya bei za mafuta.
Kupunguza vichafuzi vya muda mfupi kama methane kunaweza kupunguza ongezeko la joto, uchafuzi wa hewa, na kusaidia mpango wa kupunguza kaboni kwa gharama nafuu, hasa katika sekta ya mafuta na gesi. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha wafanyakazi na jamii zinazotegemea sekta za kaboni hawaachwi nyuma.
COP30 inatarajiwa kuidhinisha mfumo wa hatua wa Belém kwa mabadliko ya haki, utakaoelekeza jinsi serikali na sekta binafsi zitakavyoweka watu katikati ya mabadiliko ya kiuchumi kupitia uundaji wa ajira, mafunzo, na mikakati ya utofauti wa uchumi.
6. Jinsi ya kurejesha ari ya Paris
Wakati mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi ulipitishwa mwaka 2015, uliibua matumaini kwamba binadamu wangeweza kubadilisha mkondo wa mabadiliko ya tabianchi. Bila mkataba huo, dunia ingekuwa kwenye njia ya kuongezeka kwa joto kwa nyuzi 3–3.5°C. Leo, dunia inaelekea nyuzi 2.3–2.5°C, ingawa bado kiwango hicho kinaweza kuwa na madhara makubwa kwa mabilioni ya watu.
Ndiyo maana wengi wanasema COP30 lazima ifufue ari ya Paris ya mwaka 2015, na kuanzisha “muongo wa utekelezaji” ambapo ahadi za hali ya hewa zinageuzwa kuwa vitendo halisi duniani.
“Kuna muda bado kwa binadamu kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, lakini tunapaswa kuchukua hatua sasa na kwa uamuzi kama tulivyofanya miaka kumi iliyopita.” amesema Ruth Do Coutto wa UNEP.