
Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani amesema, ataanza kufanya mazungumzo hivi karibuni kwa ajili ya kuunda serikali mpya wakati muungano wake unaonekana kuongoza katika uchaguzi wa bunge.
Katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni, al-Sudani amesema muungano wake wa Ujenzi Mpya na Maendeleo umeongoza katika uchaguzi wa bunge na “utabaki hivyo.”
Ameahidi kwamba serikali ijayo “itawahudumia Wairaqi wote na kulinda maslahi ya kila mtu, ikiwa ni pamoja na wale waliochagua kususia uchaguzi.”
“Iraq ni ya wote na itabaki kuwa ya wote,” amesisitiza waziri mkuu huyo aliyemaliza muhula uliopita wa uongozi.
“Tunatoa wito kwa kila mtu kuweka maslahi ya Iraq juu ya maslahi mengine yote na kuheshimu matakwa ya wapiga kura,” ameeleza al-Sudani.
Amebainisha kuwa, hatua inayofuata itajikita kwenye mazungumzo yatakayofanywa kwa moyo wa uunganishaji na uwajibikaji kitaifa, yakilenga kubuni muundo wa serikali mpya; serikali ambayo ina sifa na uwezo wa kutekeleza programu na ahadi zake.
Waziri Mkuu wa Iraq amesema katika hotuba yake hiyo kwamba, muungano wake “uko wazi kwa pande zote bila kumtenga yeyote.”
Al-Sudani amesisitiza pia kwa kusema: “lengo letu ni kujenga uelewa imara unaoheshimu katiba na kudhamini ushiriki wa dhati, kwa watu wote katika ufanyaji maamuzi”.
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Iraq (IHEC) yameonyesha kuwa muungano wa al-Sudani umeongoza katika mji mkuu Baghdad kwa kunyakua kura 411,026.
Tume hiyo imesema, idadi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura nchini kote ilifikia 56.11%…/