Vita nchini Sudan vimechukua sura mpya kufuatia kuendelea uingiliaji kati wa nchi ajinabi nchini humo na kudhibitiwa mji wa Al Fasher na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Mamia ya watu wameuawa na ripoti zinaarifu kunyongwa watu na kujiri mauaji ya halaiki katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kufuatia kudhibitiwa mji wa Al Fasher na wanamgambo wa ESF. Hii ni katika hali ambayo Minni Arko Minnawi Gavana wa Darfur na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Sudan ametupa ujumbe katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: Zaidi ya asilimia 85 ya wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ni mamluki kutoka nje. Wengi wanaweza wasijue ukweli lakini unadhihirishanaman kundi hilo lisivyo la kizalendo na tishio kubwa kwa mustakabali na umoja  wa Sudan. Minnawi ameeleza kuwa wanapasa kukabiliana na uingiliaji wa pande na nchi ajinabi katka vita vya ndani vinavyojiri Sudan na kusisitiza kuwa umoja wa kitaifa unapasa kuimarishwa katika jeshi la Sudan  ili kulinda mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. 

Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, zaidi ya watu 150,000 wamepoteza maisha katika mapigano nchini Sudan na takriban watu milioni 12 wameyakimbia makazi yao katika kile kilichotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa maafa makubwa zaidi ya binadamu duniani.

Baada ya kutekwa mji wa Al Fasher na kikosi cha RSF; mustakbali wa Sudan ambayo wakati fulani ilikuwa ikijulikana kama nchi kubwa zaidi na kapu la chakula la Ulimwengu wa Kiarabu ipo hatarini huku weledi wengi wa mambo wakitahadharisha kuhusu hatari ya kujitenga maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo.  Kuanguka Al Fasher mji ambao ulikuwa kituo kikuu cha mwisho cha kanda nje ya udhibiti wa RSF, ni tukio la kijiografia na kubwa; na wakati huo huo ni  mwanzo wa awamu mpya ambayo, ikiwa itaendelea, itasababisha kugawanyika nchi nzima ya Sudan. Kuanguka mji wa Al Fasher mikononi mwa wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kunatoa fursa kwa kikosi hicho ya kufikia kivuko muhimu kilichoko katika mpaka kati ya Chad na Libya; huku suala la uingiliaji wa nchi ajinavi huko Sudan ikiwa ni kadhia nyeti. 

Wanamgambo wa RSF 

Kwa hakika, hali tete ya ndani ya nchi hiyo na mapigano kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSf yameibua mazingira ambayo madola ya kieneo na kimataifa yanafanya kila yawezavyo ili kuathiri matukio ya kisiasa na kijeshi huko Sudan.

Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ambacho awali kiliasisiwa kwa lengo la kukabiliana na waasi wa ndani na machafuko huko Sudan; hivi sasa kimekuwa moja ya pande kuu chezaji za kijeshi nchini humo. Aghalabu ya wanamgambo wa kundi hilo wametumwa Sudan wakitokea katika nchi jirani na Sudan kama Chad na Eritrea. Ukweli huu wa mambo unaonyesha kuwa mgogoro wa Sudan si suala la ndani tu, bali mgogoro huo umekuwa uwanja wa ushindani kati ya pande chezaj kutoka nje zikiwani kuwa na ushawishi na udhibiti huko Sudan na katika ukanda wa Kaskazini mwa Afrika.

Uingiliaji wa nchi mbalimbai ajinabi katika mgogoro wa Sudan zikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia na nchi za Magharibi kama vile Marekani na Umoja wa Ulaya pia unaonekana waziwazi. Nchi hizi zimeingia kwenye mgogoro wa Sudan kwa malengo tofauti. Kwa mfano, Imarati ambayo huko nyuma ilizidisha ushawishi wake wa kiuchumi na kisiasa nchini humo  kwa kuwekeza katika migodi ya dhahabu ya Sudan na katika rasilimali nyinginezo, inajulikana kuwa miongoni mwa wachezaji wakuu tangu kuanza kwa vita huko Sudan. Imarati imekuwa ikikipatia kikosi cha wanangambo wa RSF   aina mbalimbali za silaha,msaada fedha na suhula za kilojistiki. 

Saudi Arabia pia inataka kuimarisha nafasi yake nchini Sudan, kwa sababu inaihesabu nchi hiyo kuwa mshirika wake wa kimkakati mbele ya vitisho vya pamoja; kwa msingi huo, kwa upande mmoja, inaliunga mkono jeshi la Sudan na, kwa upande mwingine, inajaribu kuzuia kuenea hali ya mchafukoge huko Sudan na athari zake hasi kwa usalama wa kikanda. 

Mbali na uingiliaji kati wa kikanda, madola makubwa duniani pia yanahusika katika mgogoro wa Sudan. Uingiliaji wa  Marekani na Umoja wa Ulaya katika mgogoro wa Sudan sana sana unafanywa kwa sababu za kisiasa, kibinadamu na za kimkakati. Nchi hizi hasa baada ya kupinduliwa Omar al-Bashir mwaka 2019, zinadai kuwa zinaunga mkono suala la kukabidhi madaraka nchini Sudan na kurejesha demokrasia na utawala wa sheria nchini humo. Wakati huo huo Washington na Brussels zimesema kuwa zina wasi wasi kuhusu kuenea machafuko ya Sudan katika nchi jirani na vitisho vya  makundi ya kigaidi katika eneo. Pamoja na hayo, uingiliaji wa nchi ajinabi umeshadidisha mgogoro wa ndani na kusababisha migawanyiko zaidi huko Sudan. 

Omar Hassan al Bashir 

Vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan sasa vimekuwa nyeti kwa ajili ya  mustakabali wa nchi hiyo na eneo zima kwa ujumla. Wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ambao wanaungwa mkono pakubwa kutoka nje ni tishio kubwa kwa umoja wa Sudan. Kundi hilo linafanya kila liwezalo ili si tu liliimarishe zaidi ushawishi wake bali hata liandae mazingira ya kusambaratika Sudan; nchi tajiri yenye nafasi ya kijiopolitiki. Dalia Abdulmunim mchambulzi wa siasa za Sudan anasema: Hii ni vita ya maamuzi. Kikosi cha RSF kinaweza kutangaza uhuru au kushinikiza kuganywa Sudan.

Katika hali kama hii, inaonekana kuwa upo udharura wa kukomeshwa kikalifu uingiaji wa nchi za nje katika masuala ya Sudan na Wasudani wenyewe watafute njia za kutatua mgogoro unaoisibu nchi yao ili kurejea katika amani ya kudumu.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *