
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika mkutano huo mabadiliko ya tabianchi yanachochea watu kufurushwa makwao na kuendelea kuwalazimisha kuwa wakimbizi hasa wale ambao tayari walikimbia kutokana na migogoro.
Shirika hilo pia linaeleza kuwa wakimbizi wengi na watu waliokimbia makazi yao wanaishi katika nchi zenye hatari kubwa zinazohusiana na tabianchi, na makazi ya wakimbizi yako katika hatari ya kutofaa watu kuishi kutokana na masuala kama joto kali na uhaba wa maji.
Akizungumza na UN News katika mkutano huo Alifonso Herrera balozi mwema wa UNHCR amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu hasa kwa wakimbizi
“Ninafurahia juhudi hii hasa kwa sababu tunapozungumza kuhusu mzozo wa tabianchi, tunapozungumza kuhusu wakimbizi waliopata madhara ya janga la tabianchi, tunazungumzia sauti ambazo hazijasikika, na hii ni fursa kwao kuzungumza kuhusu mambo muhimu yanayowaathiri.”
Herrera, mwigizaji nyota wa Mexico na balozi mwema wa UNHCR tangu 2020, yupo Belém kueneza uelewa kuhusu uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na watu waliolazimika kukimbia makazi yao. Ameipongeza Brazil kwa ukarimu wake kwa wakimbizi, akibainisha tofauti na nchi nyingine ambazo haziko tayari kutoa msaada kwa watu waliokimbia makwao
“Ninafurahishwa na unyumbulifu na ukarimu ambao Brazil inaonesha kwa watu hawa, hasa ikizingatiwa maamuzi ya nchi nyingine ambazo haziko tayari au haziko wazi kama Brazil.”
Mkutano huo unafanyika karibu na eneo la Amazon, ambalo ni muhimu sana katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Herrera, anasema alikuwa hapo yapata miongo miwili iliyopita, na uzuri wa uhifadhi wa maziringa alioona bado upo hadi sasa.
“Ni eneo zuri. Nimekuwa Manaus mwaka 2006, Belém mwaka 2007 ni furaha kubwa kuwa katika eneo hili tena. Ninafurahi sana kuwa Brazil na katika Eneo la Amazon.”
COP30 inaendelea tena wiki ijayo, sauti kama ya Herrera inakumbusha dunia katika upande wa kibinadamu kuchukua dhidi ya tabianchi sasa na kwamba wale walioathirika zaidi wanastahili kusikika.