
Nchini Mali, idadi ya wageni wanaotekwa na wanajihadi imeendelea kukuwa. Shirika lisilo la kiserikali la ACLED, ambalo hufuatilia vitendo vya vurugu katika maeneo ya migogoro duniani kote, linaonyesha kwamba angalau wageni 22 walikamatwa na kuchukuliwa mateka na JNIM, shirika tanzu la al-Qaeda, katika miezi sita iliyopita. Rekodi hii mbaya na ya kusikitisha inaangazia hali ya usalama nchini na mkakati wa wanajihadi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kati ya mwezi Mei na Oktoba, angalau raia wa kigeni 22, labda hadi 26, walichukuliwa mateka na JNIM nchini Mali. Ingawa baadhi ya visa bado havijaeleweka, hitimisho ni lile lile kwa Héni Nsaibia, mtaalamu wa Sahel katika ACLED: hii ni “karibu mara mbili ya rekodi ya awali iliyowekwa mwaka wa 2022,” wakati raia wa kiwageni 13 walitekwa nyara.
Fidia, chanzo cha ufadhili
Katika miezi sita iliyopita, JNIM imewakamata raia wa China, India, Misri, Imarati, Iran, Serbia, Croatia, na Bosnia. Baadhi wameachiliwa, lakini si wote. Shirika lisilo la kiserikali la ACLED linasema kwamba halina taarifa sahihi na zilizothibitishwa vya kutosha kutoa takwimu kuhusu kutolewa kwa watu hao. “Utata” huu unahusu hasa raia wa China na India.
Matekaji hao kwa ujumla walikamatwa katika maeneo ya viwanda au migodi kusini mwa nchi. Fidia zimekuwa chanzo cha ufadhili kwa wanajihadi. Mwishoni mwa mwezi Oktoba, angalau dola milioni 50 zililipwa kwa JNIM—rekodi nyingine—badala ya mateka wa Imarati na wenzake; Mpakistani na Mhindi walikamatwa na kuachiliwa wakati mmoja na jenerali wa Imarati.
“Kuzuia uwekezaji wa kigeni”
Lakini utekaji nyara huu mwingi pia ni sehemu ya mkakati mpya wa kuidhoofisha nchi kiuchumi. Tangu mwanzoni mwa mwezi wa Septemba, JNIM imekuwa ikifanya kazi ya kudumisha uhaba wa mafuta nchini Mali, na kudhoofisha shughuli nyingi. “Wanaua ndege wawili kwa jiwe moja,” anachambua Heni Nsaibia wa ACLED, ambaye anaelezea kwamba ongezeko la utekaji nyara pia linalenga “kuzuia uwekezaji wa kigeni na ushirikiano wa kiuchumi na serikali.”
Mbali na raia wa kiwageni, JNIM inawashikilia mateka kadhaa, raia wa Mali: wanajeshi, wawakilishi wa serikali, au raia wa kawaida. Idadi yao halisi haijulikani.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop alisema kwamba “mabadiliko katika mfumo wa utendaji kazi wa magaidi” yalikuwa “ishara ya kudhoofika kwao.”
Ikumbukwe kwamba kundi la Islamic State huko Sahel (ISS), kundi la wanajihadi linalochukuliwa kuwa “mpinzani” wa JNIM, pia lipo nchini Mali, lakini halijawateka nyara raia wowote wa kigeni huko. Hata hivyo, ISIS imewateka nyara raia wa kiwageni 12 huko Niger na Burkina Faso, na mmoja huko Algeria, katika miezi ya hivi karibuni, kulingana na ACLED.