
Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo OCHA imesema hali imezidi kuwa mbaya haraka baada ya mashirika ya kibinadamu kulazimika kusitisha shughuli za usimamizi wa kambi mwezi Oktoba kutokana na upungufu mkubwa wa fedha.
Huduma hizi zilikuwa muhimu kwa uendeshaji wa kambi, kuhakikisha usalama kwa watu waliokimbia, na kuratibu msaada muhimu kama vile maji safi, usafi wa mazingira, huduma za afya, elimu ya dharura na makazi.
Familia za wakimbizi ziko hatarini
“Bila wasimamizi wa kambi, familia zilizokimbia zinabaki hatarini kutokana na vitisho vinavyoweza kuzuilika,” OCHA imeonya, ikiongeza kuwa kusitishwa kwa uangalizi wa kambi kunaharibu utoaji wa msaada wa dharura kwa uwiano na uwajibikaji.
Shirika hilo limetoa wito wa dharura kwa wafadhili na washirika wa kimataifa kuhamasisha rasilimali ili kurejesha huduma muhimu na kuzuia madhara zaidi kwa jamii zilizo hatarini.
Mamlaka za serikali zinakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 1 bado wamekimbia makazi yao katika jimbo la Ituri kufikia mwisho wa Oktoba, huku usalama na mahitaji ya kibinadamu yakizidi rasilimali zilizopo.