Sababu ya watu kukwama ni kwamba wapiganaji wa vikosi vya wanamgambo wa Msaada wa Haraka waliteka mji huo, na hivyo kuvamia na kuudhibiti baada ya mzingiro wa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, wakazi wengi wameachwa bila njia ya kutoroka.

“Mateso hayo yaliwalazimisha watu kula maganda ya karanga na chakula cha mifugo,” amesema leo Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, kabla ya kulaani mauaji ya halaiki ya raia, watu kuuawa kwa misingi ya kabila na ukatili mwingine unaoendelea kufanywa.

Msaada unatayarishwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika kambi ya Zamzam huko Tawila, Darfur Kaskazini.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Msaada unatayarishwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika kambi ya Zamzam huko Tawila, Darfur Kaskazini.

Katika Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi, Bwana. Türk amewaambia wanachama kuwa hata madoa ya damu ardhini El Fasher yanaonekana kutoka angani.

“Tulionya kwamba kuanguka kwa mji huo mikononi mwa Rapid Support Forces RSF, kungesababisha umwagaji mkubwa wa damu,” amesema, akitoa wito kwa hatua za haraka za kimataifa kusitisha ghasia katika kikao maalum kilichoitishwa na nchi wanachama wenye wasiwasi. 

“Wote wanaohusika na mzozo huu wanapaswa kujua kwamba tunawaangalia na haki lazima itendeke,” amesisitiza Kamishna Mkuu.

Wamekwama wakitafuta msaada

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), “karibu watu 100,000 wamekimbia El Fasher na vijiji vya karibu katika wiki mbili zilizopita pekee.

Wamekwama mahali fulani. Familia zinazowasili Tawila, takribani kilomita 50 kutoka El Fasher, zimeripoti hofu zisizofikirika walizopitia kabla na baada ya kutoroka mji huo.” Amesema Jacqueline Wilma Parlevliet, Mkuu wa Ofisi ndogo ya UNHCR huko Port Sudan

Akizungumza na wanahabari kwa njia ya video kutoka Geneva, Bi. Parlevliet amesema kuna taarifa nyingi za ubakaji na ukatili wa kingono kwa waliokimbia, pamoja na hali ya kukata tamaa.

“Wazazi wanatafuta watoto wao waliopotea, wengi wakiwa wamepata mshtuko kutokana na vita na safari hatari ya kutafuta usalama. Kwa kukosa pesa za kulipa fidia, familia zimewapoteza vijana wao kwa kukamatwa au kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha,” ameeleza.

Wale wanaojaribu kupata usalama nje ya El Fasher wanazidi kukabili safari hatari, wakiepuka vizuizi vya kijeshi, baadhi wakisafiri hadi siku 15 bila chakula na maji ya kutosha kabla ya kufika maeneo ya hifadhi kama Ad Dabbah katika jimbo la Kaskazini.

Mji mdogo uliopo kingo za Mto Nile sasa unahifadhi angalau watu 37,000 kutoka El Fasher na maelfu wengine wanatarajiwa kuwasili. Ripoti pia zinaonesha kuwa makundi yenye silaha yanawalazimisha watu wengi kurudi El Fasher ambako hali ni mbaya mno, kwa mujibu wa UNHCR ikinukuu vyanzo vya eneo hilo.

“Maelfu ya watu, hasa wazee, watu wenye ulemavu na majeruhi, bado wamekwama, ama wanazuiwa kuondoka au hawana uwezo wa kutoroka,” amesema Bi. Parlevliet.

Watoto waliokimbia ghasia huko El Fasher wanapokea vifaa vya shule huko Tawila.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Watoto waliokimbia ghasia huko El Fasher wanapokea vifaa vya shule huko Tawila.

Mgogoro wa kiwango cha kutisha

Sudan ndiyo nchi yenye mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani, zaidi ya watu milioni 12 wakiwa wamekimbia makazi yao ndani na nje ya nchi.

Kwa wengi wanaojaribu kurejea makwao katika maeneo mengine ya taifa hilo kubwa la Afrika Mashariki, tishio la mabomu ambayo hayajalipuka ni kubwa sana, kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa kutegua mabomu (UNMAS).

Lilisema kuwa katika majimbo ya Kordofan Kusini, Kordofan Magharibi na Blue Nile pekee, kilomita za mraba milioni 13 za ardhi zimeathiriwa.

“Kuna nchi nyingi zilizoathiriwa na mabaki ya mabomu ya vita. Lakini Sudan ni tofauti. Kwa nini? Kwa sababu vita vinafanyika mijini,” amesema Sediq Rashid, Mkuu wa UNMAS Sudan, akizungumza kutoka Port Sudan.

Amesema kuwa hata katika mji mkuu Khartoum, hatari zinajumuisha mabomu ambayo hayajalipuka, risasi zilizotelekezwa, mabomu ya kuzuia magari na yale ya ardhini kwa binadamu.

Ameongeza  kueleza kuwa familia zilizokimbia makazi yao ziko kwenye hatari zaidi, mara nyingi zikijikuta kwenye maeneo wasiyoyajua bila ufahamu wa migogoro ya awali au maeneo yaliyoathiriwa

“Wakati huo huo, vifo na majeruhi ambao ni  raia kutokana na mabomu ya ardhini vinaendelea kuongezeka na tunajua kwamba visa vinavyoripotiwa ni sehemu ndogo tu ya madhara halisi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *