India. Nchini India katika tasnia ya filamu, jina la Indravadan Purohit halisikiki sana, tofauti na mastaa wakubwa kama kina Salman Khan na Shah Rukh Khan. Lakini nyuma ya pazia Purohit ndiye aliyeubeba uhusika ambao ulikubalika na mamilioni ya watu duniani, akiigiza kama Jadoo wa Koi… Mil Gaya.
Indravadan alizaliwa miaka ya 1950, katika familia ya kawaida kabisa nchini India. Akiwa na umbile dogo maisha yake hayakuwa mepesi huku baadhi ya watu wakimwona kama kikwazo na mzigo ambao mara zote ulihitaji kubebwa (kusaidia).
Kwa upande wake, alichukulia hali yake ya kama fursa na tiketi ya kuingia kwenye uigizaji. Akiwa bado kijana alianza kama msanii wa ‘stage shows’ kabla ya kuingia kwenye filamu za Kihindi, Gujarati na Rajasthani.
Taratibu alijizolea umaarufu kutokana na uwezo wake wa kuigiza bila kutegemea sauti au kuonekana kwa sura, bali kupitia mwili na mwendo wake (body acting), jambo lililomfanya atambulike kama mtaalamu mahiri wa “suit acting”.
Mwaka 2002, timu ya utayarishaji wa filamu Koi… Mil Gaya ikiongozwa na Rakesh Roshan ilihitaji msanii atakayeweza kuigiza ndani ya ‘full body suit’ ya kiumbe wa ajabu, ‘Jadoo’ kiumbe ambaye anauwezo wa kuteka hisia za watazamaji wa filamu husika bila ya kuzungumza.
Wakati wanatafuta muhusika wa Jadoo, Rakesh alitoa vigezo ambapo mtu huyo alitakiwa kuwa mwenye kimo kifupi. Lakini pia awe na uvumilivu wa kufanya kazi kwsa muda mrefu akiwa ndani ya vazi lenye uzito zaidi ya kilo 20, kuhimili joto kwa muda mrefu pamoja na kujua kuchezesha mwili wake vizuri (body language).
Aidha, bahati hiyo ilimwangukia Indravadan Purohit ambapo alichaguliwa kwa sababu ya uzoefu wake mkubwa katika suit acting. Uwezo wake wa kutumia mwili katika kuigiza na nidhamu aliyokuwa nayo.
Kama ilivyo kwa wasanii wengi ambao huwepo nyuma ya pazia, jina lake halikuwahi kutajwa sana kwenye tuzo. Lakini alijizolea umarufu mkubwa katika tasnia ya filamu nchini India huku wengi wakimtambulisha kama mwalimu wa ‘Suit Acting’, akionekana kwenye filamu mbalimbali kama Aakhri Daku, Veerana, Paap Ki Duniya, Mard, Taqdeerwala na nyingine nyingi.
Indravadan Purohit, ambaye wengi wanamkumbuka kama Jadoo wa kwenye Koi… Mil Gaya, alifariki dunia Septemba 28, 2014 huku sababu ya kifo chake ilitajwa kuwa ni viungo vyake vya mwili kushindwa kufanya kazi (multiple organ failure).
Utakumbuka filamu ya Koi… Mil Gaya iliachiwa rasmi Agosti 8, 2003 huku muhusika mkuu akiwa ni Hrithik Roshan ambaye aliigiza kama Rohit. Vazi la Jadoo katika filamu Koi… Mil Gaya lilitengenezwa na James Colmer, kazi hiyo ilifanywa nchini Australia, na ilichukua zaidi ya mwaka kuunda costume nzima ya Jadoo.