“Usiku wa kuamkia leo Novemba 19, mashambulizi mengine yaliyofanywa na Jeshi la Shirikisho la Urusi yameua takriban raia 20 na kuwajeruhi zaidi ya mia moja, wakiwemo watoto,” kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kuratibu mMasuala ya Kibinadamu OCHA.

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu, nchini Ukraine Matthias Schmale, amelaani vikali mashambulizi hayo.

OCHA imesema kuwa makazi ya watu na miundombinu muhimu ya kiraia ikiwa ni pamoja na vituo vya afya na taasisi za elimu vimeharibiwa vibaya katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Watu wameuawa kila kona

Kutoka Kharkiv upande wa mashariki hadi Ternopil na eneo la Ivano-Frankivsk magharibi mwa Ukraine, OCHA imesema familia zimepoteza wapendwa wao, wengine wamejeruhiwa, na wengi wameachwa bila makazi.

Inaripotiwa kuwa angalau watoto kadhaa ni miongoni mwa waathiriwa. “Mateso yao hayana kificho wala uhalali,” imesema OCHA nchini Ukraine.

Mashambulizi hayo pia yameharibu miundombinu ya nishati, na kusababisha kukatika kwa umeme, jambo linaloongeza athari za mashambulizi ya awali. Kwa mujibu wa OCHA Kukatika huko kwa umeme ni tishio kubwa kwa mamilioni ya watu, hasa wakati ambapo katika baadhi ya maeneo joto limeshuka chini ya kiwango cha kuganda.

Taarifa hiyo ya OCHA imesisitiza kuwa “Tishio hili linaloendelea kwa raia na uharibifu wa miundombinu muhimu ya kiraia ni jambo lisilokubalika kabisa. Kuwalenga raia au vitu vinavyohitajika kwa ajili ya kuendeleza maisha yao ni marufuku chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.”

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, ametoa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mchana huu kuhusu mashambulizi hayo

Amesema “Katibu Mkuu analaani vikali mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyofanywa usiku wa kuamkia leo na Shirikisho la Urusi katika maeneo kadhaa ya Ukraine, ambayo yameripotiwa kuua angalau watu 25, wakiwemo watoto watatu, na kuwajeruhi wengine kadhaa katika majengo mawili ya makazi mjini Ternopil, magharibi mwa Ukraine.”

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanakiuka sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Hayakubaliki, popote yanapotokea, na yanapaswa kusitishwa mara moja.

Shambulio hili la kutisha imesema taarifa ni moja ya mabaya zaidi dhidi ya raia tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza kwa kiwango kikubwa karibu miaka minne iliyopita na linathibitisha tena umuhimu wa usitishaji mapigano wa haraka, kamili na usio na masharti.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa “Huu ni msingi muhimu kuelekea amani ya haki, ya kina na endelevu inayolinda kikamilifu uhuru, kujitegemea na uadilifu wa eneo la Ukraine ndani ya mipaka yake inayotambuliwa kimataifa, kulingana na Mkataba wa UN, sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.”

Umoja wa Mataifa umezitaka pande zote katika mzozo zitumie kila njia kulinda raia wa Ukraine na kusisitiza kuwa raia “hawapaswi kamwe kulengwa katika mashambulizi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *