
Maudhui ya siku ya choo duniani mwaka huu ni “Siku zote kila mtu atahitaji kuduma ya choo, usafi katika dunia inayobadilika”, kwa mujibu wa Dkt. Rüdiger Krech, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi, fya Moja na Uhamaji katika shirika la WHO. “Usafi salama ni msingi wa afya na utu wa binadamu. Katika kila jamii, choo hulinda watu dhidi ya magonjwa, hulinda mazingira yetu na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”
Licha ya hatua zilizopigwa katika miongo iliyopita, WHO inasema watu bilioni 3.4 duniani kote bado hawana huduma salama ya vyoo, hali inayoziacha familia katika hatari ya magonjwa hatarishi.
Ukosefu wa huduma za maji safi, usafi wa mazingira na unawaji mikono yaani WASH shirika hilo limesema husababisha vifo milioni 1.4 kila mwaka, huku magonjwa ya kuhara yakiwa zaidi ya theluthi mbili ya mzigo huo.
WHO imebainisha kuwa takribani watoto 1,000 wa chini ya umri wa miaka mitano hufariki kila siku kutokana na magonjwa yanayohusiana na huduma duni za WASH.
“Hili ni janga linaloweza kuzuilika na linaloweza kutatuliwa,” amesisitiza Dkt. Krech.
Pia WHO imeonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza changamoto za usafi wa mazingira, kwani mafuriko na ukame huharibu miundombinu na kuchafua vyanzo vya maji.
Imesisitiza kuwa “Wale walio katika mazingira hatarishi ndio wanaoathirika zaidi. Kujenga huduma imara za usafi wa mazingira si hiari tena ni jukumu muhimu la afya ya umma na njia ya kujiandaa na mabadiliko ya tabianchi.”
Shirika hilo limesema mikakati madhubuti inajulikana ambayo ni uwekezaji endelevu wa umma, usimamizi thabiti, na takwimu za kuaminika.
Limeongeza kuwa vituo vya afya pia vina umuhimu mkubwa. “Hakuna hospitali au kliniki inayoweza kuwalinda wagonjwa na wahudumu wa afya bila maji safi, usafi wa mazingira na unawaji mikono. Mifumo hii ni muhimu katika kupunguza maambukizi, vijidudu na usugu wa viuatilifu.”
WHO inasisitiza kuwa usafi wa mazingira ni haki ya binadamu, na imetoa wito kwa serikali kuhakikisha vyoo vinakuwa imara, vinapatikana kwa wote, na ni vya gharama nafuu ikiwemo kwa wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na jamii zilizo katika maeneo yenye hali tete.
Dkt. Krech amesisitiza “Hili si tu kuwa na sera nzuri ni wajibu wa kimaadili. Nchi zinapotekeleza mipango ya muda mrefu, ushirikiano wa sekta mbalimbali na uwajibikaji, faida za kiafya, kiuchumi na kijamii ni kubwa.”
Dunia ikiadhimisha Siku ya Choo Duniani, WHO imezitaka nchi kuongeza kasi ya maendeleo ikisema “Tuwekeze katika vyoo vyenye uimara kwa ajili ya siku zijazo, na kuhakikisha kila mtu, kila mahali, anapata usafi salama. Pamoja, tunaweza kuzuia magonjwa, kulinda sayari yetu na kuimarisha utu wa kila mtu.”