Katika mkutano huo Guterres amesema kuwa anamshukuru Rais Cyril Ramaphosa na watu wa Afrika Kusini kwa mapokezi mazuri na kwa kuandaa Mkutano wa G20. Amesema kwamba ujumbe wake kwa viongozi wa G20 katika siku mbili zinazofuata ni rahisi, “huu ni wakati wa uongozi na maono.”
Ameeleza kuwa dunia inapitia nyakati zenye misukosuko, ikijumuisha migogoro, mgogoro wa tabianchi, ukosefu wa uhakika wa kiuchumi, ongezeko la deni, na kuporomoka kwa misaada ya kimataifa vitu ambavyo vinasababisha mateso makubwa duniani. Ameongeza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi kunapunguza rasilimali zinazohitajika kwa maendeleo.
Guterres amesisitiza kwamba kama uchumi mkubwa duniani, nchi za G20 zina ushawishi mkubwa wa kupunguza mateso, kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wote, na kuelekeza dunia kwenye njia bora na ya amani zaidi. Amesema kuwa kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu “Ushikamano, Usawa na Uendelevu” inaonesha mwelekeo sahihi.
Ameendelea kueleza kuwa katika siku mbili zijazo, atatoa wito kwa nchi wanachama wa G20 kutumia ushawishi wao kuongoza hatua zinazohitajika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wanahabari katika Mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini.
1. Hatua za Kiuchumi
Guterres amesema kuwa nchi zinazoendelea hasa barani Afrika zinateseka kutokana na “dhoruba kamili” ya upungufu wa uwezo wa kifedha, mizigo mikubwa ya madeni, na mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao hauwasaidii wala kuwakilisha ipasavyo.
Amesema, “Afrika imekuwa mwathiriwa mara mbili wa ukoloni kwanza kwa karne za unyonyaji, na pili wakati taasisi za kimataifa zikiundwa bila uwepo wa sauti za mataifa ya Afrika yaliyokuwa chini ya ukoloni.” Ameongeza kuwa bara hilo bado halijawakilishwa vya kutosha katika taasisi za kimataifa, na kwamba hali hii lazima ibadilike.
Katibu Mkuu amekumbusha kuwa Pact for the Future iliyopitishwa mwaka uliopita ilitaka mageuzi ya taasisi za fedha za kimataifa, ambapo maamuzi mengi yanachukuliwa na baadhi ya wanachama wa G20. Amesema “Afrika inapaswa kuwa na nafasi ya haki katika kila jukwaa la maamuzi kuanzia bodi za taasisi za fedha za kimataifa hadi viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”
Katibu Mkuu ameongeza kuwa G20 inaweza kusaidia kurekebisha dhuluma ya kihistoria na kuendesha mageuzi yatakayowapa nchi zinazoendelea hasa Afrika sauti ya kweli katika kutengeneza sera za dunia. Vilevile, ametoa wito kwa nchi za G20 “kutekeleza ahadi za Mkutano wa ufadhili kwa ajili ya maendeleo uliofanyika Sevilla mwezi Juni.”
Amewataka kuongeza uwezo wa kukopesha wa benki za maendeleo, kuimarisha upatikanaji wa fedha binafsi, kupunguza mizigo ya madeni, na kusaidia nchi zinazoendelea kuongeza uwezo wao wa kukusanya rasilimali za ndani. Amesema kuwa G20 inaweza kuvunja vizuizi vya kibiashara ili nchi masikini ziweze kupata masoko yao bila vikwazo.
Ameonya kuwa usawa umegeuka kuwa “saratani katika jamii nyingi, ukikusanya mamlaka na kudhoofisha imani katika demokrasia.
Dhoruba za mchanga na vumbi huathiri jamii huko Garissa, kaskazini mwa Kenya.
2. Hatua za kukabiliana na Tabianchi
Guterres amesema kuwa mkutano wa COP30 unaendelea na unaonesha kazi kubwa inayosubiriwa. Amesema kwamba dunia imeshindwa kudhibiti ongezeko la joto hadi 1.5°C, na kwamba sayansi inaonesha kupitiliza kiwango hicho kwa muda ni jambo lisiloepukika na kwamba lazima kupitiliza huko kuwe dogo, la muda mfupi na salama.
Ametoa wito wa kuziba pengo la kurekebisha mifumo ili kukabiliana na mabadiliko yanayotokea. haraka, akisisitiza mahitaji makubwa ya ufadhili. Amewakumbusha nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao ikiwa ni pamoja na kuongeza fedha za mnepo hadi dola bilioni 40 mwaka huu, na kuhakikisha upatikanaji wa dola bilioni 300 kwa mwaka ifikapo 2035.
Pia ametaja mpango wa Baku hadi Belem wa kufikia dola trilioni 1.3 kila mwaka kwa ufadhili wa tabianchi kwa nchi zinazoendelea, sambamba na kuchangia Mfuko wa Hasara na Uharibifu.
Bwana Guterres amesema “mabadiliko ya haki kuelekea nishati mbadala lazima yatiwe kasi. Ingawa uwekezaji wa kimataifa wa nishati safi umeongezeka, sehemu ndogo sana inaenda Afrika.” Amesisitiza kuwa Afrika inapaswa kuwa kitovu cha mageuzi ya nishati safi kutokana na uwezo wake mkubwa wa jua na upepo, akiongeza kuwa kuwa mpito wa haki wa nishati una maana ya kusambaza umeme barani Afrika lote kwa nyumba, shule, hospitali, viwanda na kuunda ajira kwa vijana.
Ameonya kuwa hakuna anayeweza kuachwa gizani katika zama za nishati safi, hasa bara ambalo limechangia kidogo sana katika mzozo wa tabianchi.
Katibu Mkuu huyo ametaja kwamba viashiria vya kiuchumi vinaunga mkono mpito huo, lakini utashi wa kisiasa bado uko nyuma, huku ruzuku za mafuta ya kisukuku zikiendelea na makampuni kunufaika na hali ya uharibifu wa tabianchi.
Ili kusaidia kupunguza mivutano na kuboresha maisha, walinda amani wa UNMISS wa India waliendesha kambi za mifugo katika Jimbo la Jonglei ili kutibu magonjwa, walitoa huduma za kinga na dawa bila malipo.
3. Hatua kwa Ajili ya Amani
Bwana Guterres amesema kuwa anawaomba viongozi wa G20 kutumia ushawishi wao kumaliza migogoro inayosababisha vifo, uharibifu na kuyumbisha dunia. Ametaja haja ya:
- Amani nchini Sudan kupitia kusitisha mapigano mara moja, kufikisha misaada kwa raia, kukomesha mtiririko wa silaha na wapiganaji, na kuwaleta pande zinazohasimiana mezani.
- Amani katika DRC kwa kuheshimu ardhi na mipaka ya taifa na kushughulikia mizizi ya machafuko.
- Amani na usalama katika Sahel, akionya kuwa makundi yenye silaha yanafaidika na udhaifu wa utawala na migogoro baina ya jamii.
- Amani ya haki, endelevu na kamilifu nchini Ukraine, kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
- Amani Gaza kupitia kuheshimu sitisho la mapigano, kumaliza ukiukaji wake, kuanzisha njia ya kisiasa kuelekea kumaliza ukaliaji, na kuhakikisha haki ya kujitawala kwa Wapalestina, ikijumuisha suluhisho la mataifa mawili.
Katibu Mkuu amsema kuwa sehemu zote kuanzia Haiti hadi Yemen hadi Myanmar dunia lazima ichague amani kwa misingi ya sheria za kimataifa.
Ametamatisha kwa kusema kuwa anatarajia mkutano wenye mafanikio na akawashukuru tena serikali na watu wa Afrika Kusini kwa mapokezi yao mazuri.