Video ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) inaanza kuonesha maisha ya kijiji cha Shampuyacu, katikati ya msiku wa Amazon ya Peru. Hapa, Ruth mkulima kutoka jamii ya Awajún anamkaribisha mhamasishaji wa masuala ya chakula, Waldir Maqque, na kumuonesha shamba lake la kakao pamoja na mbinu wanazotumia kuongeza thamani ya zao hilo na kulinda mazingira.

Kwa miaka ya hivi karibuni, mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa kakao nchini Peru, licha ya kuwa kati ya wazalishaji kumi wakubwa duniani. Kupanda kwa Joto na mvua kutotabirika kumewalazimu wakulima kubadilisha mbinu zao za kilimo, na ndiyo maana IFAD kupitia mradi wa AVANZAR Rural umeingilia kati kuwasaidia.

Kupitia mafunzo na vifaa vipya vinavyofadhiliwa na IFAD na Serikali ya Peru, vyama vya ushirika kama Jembe Bakau Conasha ambapo Ruth ni kiongozi wa chama hicho. Ruth anaanza kwa kueleza namna wanavyotumia maganda ya kakao kikamilifu.

Tunatumia si tu maganda ya kakao kama kiungo cha chakula, bali pia kutengeneza mbolea kwa mimea yetu. Yakioza yanakuwa mbolea bora iitwayo bocaChe.”

Katika ziara hiyo, Ruth anampeleka Maqque hadi jikoni na anamfundisha jinsi ya kupika Cecina Saltada con Cáscara  chakula cha kukaangwa kinachochanganya nyama  iliyokaushwa na kutunzwa, pamoja na maganda ya mmea wa kakao, na Maqque anashangazwa na ubunifu huo.

“Mapishi ya kuweza kukaanga maganda ya kakao kama haya ni jambo la kipekee. Lakini unapoyamenya, kuyatibu na yakawa laini, unaweza kuyaunganisha na vyakula vingi na kugundua ladha mpya, muundo mpya, kujifunza kupika kwa namna hii ni ajabu kweli, ajabu sana.” 

Ruth pia anasisitiza umuhimu wa kilimo mseto pamoja na utamaduni wao wa kupanda miti ili kurejesha ardhi.

“Kila mmea tunaoutumia kama mihogo, ndizi umepandwa kwa kutumia mbinu za kilimo mseto, kwa uangalifu mkubwa. Ikiwa ninahitaji kukata mti kwa matumizi fulani, basi kabla sijaukata, ni lazima tayari niwe nimepanda mwingine ili kuhakikisha kuwa rasilimali hii inaendelea kuwepo, sivyo?”

Anaonesha pia namna jamii yake inavyofanya uchavushaji wa vanilla kwa mikono kazi ngumu lakini yenye tija kubwa kiuchumi kwa familia na kijiji chao.

Wakati huo huo, huko jijini Rome, nchini Italia, Rais wa IFAD, Álvaro Lario, anasisitiza kuwa uwekezaji wa aina hii si mzigo bali ni fursa ya kiuchumi kwa nchi maskini.

“Uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi si wa kulinda tu maisha ya maskini, bali ni fursa ya kimkakati na kiuchumi vilevile. Kwa kuendeleza uzalishaji wa chakula, ajira na ukuaji, uwekezaji huu huimarisha uthabiti wa kiuchumi na kijamii.”

Mradi wa AVANZAR umewafikia zaidi ya wakulima wadogo 20,000, wakiwamo wanawake zaidi ya 12,000 ambapo zaidi ya 1,000 ni kutoka jamii za asili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *