Akizungumza kabla ya hotuba yake kwenye mkutano huo, Bi. Byanyima amesema, “Katika dunia iliyovutwa na kupasuliwa na ukosefu mkubwa wa usawa, hakuna aliye salama. Viongozi wa G20 wanahitaji kukabiliana na dharura ya ukosefu wa usawa ili kujenga dunia salama kwa wote.”

Ametoa wito wa kuundwa kwa Jopo la Kimataifa la Ukosefu wa Usawa, kwa mfano wa IPCC, ambalo litatoa mwongozo kwa serikali katika kukabiliana na tishio hili la kimataifa.

Pengo kubwa biana ya matajiri na masikini

Bi. Byanyima ni mjumbe wa Kamati Maalum ya Wataalamu Huru ya G20 kuhusu Ukosefu wa Usawa wa Kimataifa, inayoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Joseph Stiglitz.
Uchambuzi mpya wa kamati hiyo unaonesha pengo kubwa, kati ya mwaka 2000 na 2024, asilimia 1 ya matajiri zaidi duniani walijipatia asilimia 41 ya utajiri wote mpya, huku asilimia 50 ya watu wa chini wakipata asilimia 1 pekee.

Kiongozi huyo wa UNAIDS ameonya kuwa pengo hili si suala la kiuchumi tu ni hatari ya kiafya kimataifa.

Utafiti wa Baraza la Kimataifa kuhusu Ukosefu wa Usawa, unasema UKIMWI na Majanga vinaonesha kuwa nchi zenye ukosefu mkubwa wa usawa zilipata vifo zaidi vya coronavirus“>COVID-19, maambukizi zaidi ya VVU, na majanga yaliyodumu kwa muda mrefu zaidi.

Mgogoro wa madeni unaendeleza janga la UKIMWI

Byanyima pia ametaja mzigo wa madeni kama kikwazo kikubwa. Nchi za kipato cha chini na cha kati zinatumia karibu dola trilioni 3 kulipa madeni fedha ambazo anasema zinapaswa kuimarisha mifumo ya afya.

“Nchi zinazoendelea zinabana pumzi kwa mzigo wa madeni,” amesema. “Kulipa deni kunanyima serikali mapato muhimu ya kumaliza UKIMWI na kujilinda dhidi ya majanga yajayo.”

Mifano inaonesha madhara ya kibinadamu,mathalani nchini Brazil, watu wasio na elimu ya msingi walikuwa na uwezekano mkubwa wa kufa kwa COVID-19, nchini Uingereza, watu wanaoishi kwenye makazi yenye msongamano walipoteza maisha kwa kiwango cha juu zaidi.

Sifa kwa uongozi wa Afrika Kusini katika G20

Byanyima amesifu uenyekiti wa Afrika Kusini katika G20 kwa kuweka umoja, usawa na uendelevu kama msingi wa ajenda, na kwa kusukuma mbele upatikanaji wa dawa, jitihada za kupunguza mzigo wa madeni, na msukumo wa bima ya afya kwa wote ndani ya nchi.

“Rais Ramaphosa anaonyesha njia kuelekea dunia yenye usawa zaidi na salama zaidi,” amesema.

Wito wa kuchukua hatua kwa pamoja

Ujumbe wake kwa viongozi wa G20 uko bayana na wa moja kwa moja, ukosefu wa usawa si hatima ni matokeo ya maamuzi ya sera.

“Ushahidi ni dhahiri,” amesema. “Ukosefu wa usawa ni hatari kwa dunia. Lakini unaweza kushindwa ikiwa viongozi watachukua hatua kwa pamoja. Ukosefu wa usawa si majaliwa, ni chaguo baya la sera ambalo viongozi wanaweza kulifuta sasa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *