Kupitia mradi huu, miundombinu muhimu imejengwa, ikiwemo madaraja na mifereji iliyoboreshwa ambayo sasa inaongoza maji ya mvua kwa usalama mbali na makazi na mashamba. FAO inasema hatua hizi zinasaidia jamii kukabiliana si tu na mafuriko, bali pia na vipindi vya ukame. Placide K. Nshuti, Kiongozi wa Kitengo cha Uzalishaji Bora,cha FAO nchini Rwanda, anafafanua
“Ilikuwa mwezi Mei 2023 ambapo maji yalikuwa yakitoka maeneo ya milima ya volkano na kubeba mawe mazito ya lava, yakiyasukuma hadi mashambani na kusomba ardhi ya kilimo. Maji hayo mazito yalienea katika mashamba mbalimbali na kuharibu nyumba pamoja na barabara.”
Athari za mafuriko hayo bado zinawasukuma wengi kuikumbuka siku hiyo kwa maumivu. Wanafunzi walipoteza makazi, mazao na vifaa vya masomo. Esther Nyiramugisha ni miongoni mwa walioguswa moja kwa moja
“Nakumbuka vema janga hilo. Wakati huo nilikuwa kidato cha kwanza, na mafuriko yalisomba vitu vingi, ikiwemo vitabu vyangu vyote.”
Mradi wa FAO wajenga mnepo baada ya mafuriko Rwanda
Kwa kutambua ukubwa wa athari, FAO imetekeleza ujenzi wa mifereji ya kudumu ya kupitisha maji ya mafuriko pamoja na miundombinu ya kukusanya na kutumia maji ya mvua. Valere Nzeyimani, Afisa Mkuu wa Maendeleo na Usimamizi wa Maji katika Ofisi ya FAO Kanda ya Afrika, anafafanua hatua zilizochukuliwa:
“Mradi huu ulikuwa wa kujenga daraja lakini pia umelinda mifereji ya maji ya mvua. Mradi umezuia mafuriko kutoka kwenye maji ya dhoruba. Hivyo tunafurahi kwamba mradi huu hatimaye umedhihirisha matokeo chanya. Mradi huu umetoa matokeo yanayoonekana mashinani, maeneo ya vyanzo vya maji sasa yamelindwa na mifumo mipya ya ukusanyaji wa maji na kilimo cha umwagiliaji inaanzishwa.”
Kwa wakazi wa Rutsiro, mradi huu haukuwaletea tu kinga dhidi ya majanga bali pia umewapa fursa za kuboresha maisha. Kupitia ajira zilizotolewa na mradi, familia nyingi zimeweza kupata kipato cha uhakika na kukidhi mahitaji muhimu. Clementine Uwamoro mmoja wa wanufaika anasema
“Tumepata ajira kwa njia ya uhakika na tumeweza kulipa bima yetu ya afya kwa wakati.”
Kwa mujibu wa FAO kutokana na mafanikio haya, sasa jamii zinahisi usalama zaidi na zimewezeshwa, na hivyo kuwa tayari kuganga yajayo.