
Mpango huo unaweka pamoja mapendekezo makuu ya mageuzi ya UN80 ya Katibu Mkuu katika muundo mmoja ulio thabiti ili kuratibu juhudi zitakazowezesha mfumo wa Umoja wa Mataifa kutoa matokeo bora.
Mpango huo hauanzishi mapendekezo mapya, bali unaweka wazi jinsi mfumo wa Umoja wa Mataifa unavyokusudia kusonga mbele na yale ambayo tayari yapo mezani: hatua 87, zilizopangwa katika vifurushi 31 vya kazi katika maeneo matatu ya kazi, kuanzia operesheni za amani na mwitikio wa kibinadamu hadi teknolojia, huduma za pamoja, na muunganiko wa taasisi.
“Lengo lake ni kuleta muundo, uwazi, uwiano, na mfumo wa kiutendaji wa kusonga mbele na vipengele vyote vya Mpango wa UN80 na pia kuwawezesha kuona jinsi kila kipengele kitakavyosonga mbele: nani anayewajibika kwa nini, na katika muda gani,” Bwana Ryder amewaambia Nchi Wanachama wakati wa mkutano usio rasmi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Mpango wa jinsi Umoja wa Mataifa unavyobadilika
Mpango wa Utekelezaji uko katika kiini cha Mpango wa UN80, mchakato thabiti wa mageuzi wenye lengo la kuboresha mfumo wa Umoja wa Mataifa ili kila dola, uamuzi na amri viwe na matokeo makubwa zaidi kwa watu na dunia.
Mpango wa Utekelezaji unaweka pamoja maeneo haya matatu ya kazi, kuyatafsiri mapendekezo yake katika muundo unaoainisha majukumu, ratiba, na vyombo vya kiserikali vitakavyoyajadili.
“Iwapo tutaendeleza msukumo huu na kuuendea mpango huu kwa mtazamo chanya, miezi ijayo inaweza kuwa wakati wa mageuzi ya kweli,” Bwana Ryder amewaambia Nchi Wanachama.
Kutoka ripoti tatu hadi vifurushi 31 vya kazi
Kwa namna ya kiutendaji, Mpango wa Utekelezaji ni ramani ya njia. Unachukua mtandao mpana wa Mpango wa UN80 na kuupeleka katika vifurushi vya kazi, kuanzia mabadiliko madogo ya kiufundi hadi yale makubwa ya mfumo wote.
Baadhi ya vifurushi muhimu zaidi vinaelekea kwenye kile maafisa waandamizi wanaita “vipengele vikubwa” kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa ulio thabiti zaidi. Katika upande wa amani na usalama, hii inamaanisha mifano mipya ya operesheni za amani, ikijumuisha jinsi majukumu na rasilimali zinavyogawiwa kwa taasisi zilizo katika nafasi nzuri zaidi za kutekeleza. Katika upande wa kibinadamu, mpango unasukuma Mkataba Mpya wa Kibinadamu ili kurahisisha mipango ya dharura, kuunganisha minyororo ya ugavi, kupanua huduma za pamoja ili kila dola iwe na matokeo makubwa zaidi.
Kundi jingine la vifurushi linaangazia jinsi mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa unavyopangwa, likijumuisha “uhuishaji au kuleta upya” wa uwezo wa kikanda na upangaji upya wa Timu za Nchi za Umoja wa Mataifa) ili kuchanganya utaalamu na ufanisi wa gharama.
Mpango huo pia utasonga mbele kwa tathmini za uwezekano wa muunganiko kati ya UNDP na UNOPS, na UNFPA na UN Women, pamoja na mustakabali wa UNAIDS.
Kwa umuhimu wa kipekee, Mpango wa Utekelezaji unatoa kipaumbele cha juu katika kuunganisha “wezeshi wa kiutendaji” wote wanaoendeleza kazi za kila siku za mfumo wa UN: takwimu za pamoja; mifumo ya teknolojia iliyounganishwa; huduma za pamoja kwa minyororo ya ugavi na kazi za nyuma ya ofisi; na mbinu rahisi zaidi ya mafunzo na utafiti.
Kamati ya Uongozi na Kikosi Kazi katika kiini cha utekelezaji
Kamati mpya ya Uongozi, itakayokutana kila mwezi chini ya mwenyekiti Katibu Mkuu, itahakikisha mwelekeo wa kimkakati na uratibu miongoni mwa viongozi wa mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Chini yake, Kikosi Kazi cha UN80, kinachoongozwa na Bwana Ryder, kitakutana kila wiki kuratibu utekelezaji, kufuatilia ratiba, na kuandaa mapendekezo kwa ajili ya mapitio ya Kamati ya Uongozi.
“Kama kanuni ya msingi, hatua zote zitachukuliwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazohusika, kama zilivyoainishwa katika Mkataba, pamoja na uamuzi, maazimio na taratibu za kawaida za vyombo husika vya kiserikali,” amekumbusha.
Amebainisha kuwa Mpango wa Utekelezaji una mapendekezo yanayofaa katika mazingira matatu ya uamuzi: mazingira ya kwanza yanahusu mapendekezo yaliyo ndani ya mamlaka ya Katibu Mkuu; ya pili yanahusu mapendekezo yanayohitaji kazi zaidi, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa muunganiko uliobainishwa katika ripoti ya eneo la kazi la tatu; na ya tatu yanahusu mapendekezo yenye athari za kifedha zinazohusiana na bajeti za programu na bajeti za ulinzi wa amani, ambazo zinawasilishwa kwa Mkutano Mkuu kwa ajili ya mapitio na idhini.
Si suluhisho la uhaba wa fedha lakini ni sehemu ya majibu
Mpango unatekelezwa wakati ambapo mfumo wa Umoja wa Mataifa unaendelea kukabiliwa na upungufu mkubwa wa ufadhili, huku rasilimali zikikadiriwa kupungua kwa asilimia 25 (kutoka dola bilioni 66 hadi bilioni 50) mwaka 2026 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Mpango wa UN80 si suluhisho kwa janga la kifedha la mfumo wa Umoja wa Mataifa, bali ni dhamira ya kulinda athari kubwa zaidi, ikiwemo katika maeneo yaliyo hatarini zaidi.
‘Dashibodi’ ya umma kwa mageuzi tata
Jukwaa hili la mtandaoni linawezesha watumiaji kuona kwa haraka kila kifurushi cha kazi, malengo yake, uongozi wake na jinsi kinavyohusiana na ripoti tatu za kimsingi. Dashibodi itapanuliwa kwa ratiba na hatua muhimu na itahuishwa mara kwa mara kadri kazi inavyoendelea.
Kwa mpango ambao mafanikio yake yatapimwa si kwa hati mpya bali kwa athari chanya halisi duniani, Mpango wa Utekelezaji ni hatua ya mabadiliko: kutoka kwenye usanifu kwenda katika hatua ya utekelezaji ambapo maendeleo, mapungufu na matokeo yatafuatiliwa mahali pamoja.