Alizaliwa katika familia ambayo haikuamini kuwaelimisha wasichana, hivyo alilazimika kubaki nyumbani wakati kaka zake walienda shule. Na alipoenda Khartoum kuishi na mjomba wake ndipo alipata nafasi ya kusoma ila kwa muda mfupi tu.

Nililazimishwa kuolewa nikiwa na umri wa miaka 14 Hata kabla ya hapo, baadhi ya jamaa walinikemea kwa sababu tu ya kwenda shule. Nilipigania kumaliza shule ya msingi, lakini sikuweza kuendelea zaidi. amesema Awrelia

Hata hivyo, hakuwahi kupoteza imani katika elimu, hasa kwa ajili ya mabinti zake. “Natumai watakua kuwa wanawake viongozi wenye mafanikio na uwajibikaji. Lazima kuwe na mabadiliko kwa ajili ya wasichana.” Amesisitiza

Awrelia akiwa nyumbani huko Wau.

© IOM/Amber Christino

Awrelia akiwa nyumbani huko Wau.

Mjane mwenye watoto wanane

Nchini Sudan Kusini, ambako migogoro na mitazamo ya kijinsia iliyojengeka kwa vizazi imekuwa ikiathiri maisha, mabadiliko huja taratibu lakini wanawake kama Awrelia wanayaendeleza kwa ujasiri na uthabiti.

Akiwa mjane na mama wa watoto wanane, ametumia miaka mingi kuwalea watoto wake peke yake, mara nyingi katika mazingira magumu na yasiyotabirika.

Baba yao alikufa wakiwa bado wadogo sana. Mwanangu mkubwa alikuwa bado yuko shule ya msingi, Tangu wakati huo nimekuwa nikiwalea peke yangu.” Anakumbuka Awrelia

Katika maisha yake ya kila siku, Awrelia hukabili changamoto za mienendo tata ya kifamilia, uhaba wa rasilimali, na unyanyapaa  lakini haachi kupambana. Amesema kuwa, watu wanatarajia wanawake kuvumilia kimya kimya hata wanapojaribu kutafuta msaada.

Katika maeneo ya umma, changamoto huwa kubwa zaidi. Akizungumza kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake, inayoadhimishwa tarehe 25 Novemba kila mwaka, Awrelia anaeleza jinsi wanawake mara nyingi hupunguzwa thamani au kupuuzwa. “Wanasema sisi ni wanawake tu, kana kwamba sauti zetu hazina maana, Nilinyamaza kwa miaka kwa sababu niliogopa kuzungumza.” amesema.

Mafunzo ya kubadilisha maisha

Awrelia alikuwa tayari akionesha uongozi wake kupitia kupigania elimu ya watoto wake na kuimarisha familia yake hata kabla ya kuzungumza hadharani. Uongozi wake uliimarika zaidi alipojiunga na mafunzo ya uongozi wa wanawake ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) mjini Wau, ambayo ni sehemu ya programu ya kijamii inayolenga kuwawezesha wanawake kushiriki katika maamuzi. Mafunzo hayo ya siku tano yanaendeleza juhudi za vikundi vya wanawake nchini Sudan Kusini kwa kuwapa nafasi salama ya kujifunza, kutafakari na kukua pamoja.

Nimejifunza kuwa uongozi ni kuwatendea wengine haki na kutatua matatizo kwa uvumilivu,mafunzo yalinipa ujasiri wa kujisimamia. Sasa najua kuwa naweza kuongoza. Anaeleza

Aliporudi katika jamii yake, aliweka ujasiri huo katika vitendo. Kikundi chao cha wanawake kilikuwa karibu kuvunjika, lakini alikifufua. Sasa wanakutana mara kwa mara kusaidiana na kushirikiana changamoto. Ingawa wanakosa ufadhili kwa shughuli za kujipatia kipato kama ushonaji au upishi, kikundi chao kinatoa kitu kingine chenye nguvu sawa.

Takriban wanawake 1,400 kote Sudan Kusini wamefaidika na mafunzo ya uongozi.

© IOM/Geoffrey Sauke

Takriban wanawake 1,400 kote Sudan Kusini wamefaidika na mafunzo ya uongozi.

Kaya zinazoongozwa na wanawake

Katika maeneo mengi ya Sudan Kusini yaliyoathiriwa na uhamishaji, hadi asilimia 80 ya kaya zinaongozwa na wanawake. Kule Wau, Bentiu, Malakal, na maeneo mengine ambako IOM inaendesha programu, wanawake zaidi wanaibuka na kuchukua nafasi za uongozi.Wale waliokuwa wanyamavu sasa wanaongea kwenye mikutano, wanaunga mkono waathirika wa ukatili, na wanajenga mitandao ya kushirikiana uzoefu na kukua pamoja.

Awrelia ameona mabadiliko katika jinsi jamii inavyomtazama. Ameeleza kwamba watu wanamtambua sasa wakati wa mkutano ,na machifu na viongozi wa wanawake, wanataja jina lake na kumheshimu mbele ya kila mtu. Anajisikia fahari. Wanawake anaowaongoza wanamheshimu na anawathamini.

Kutoka majumbani hadi kumbi za jamii, wanawake kama Awrelia wanapata sauti zao na kubadilisha sura ya kesho kwa ajili ya mabinti zao, familia zao, na nchi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *