
Katibu Mkuu ameeleza kuwa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni janga la kimataifa, ambalo limezidishwa na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia.
“Katika zama zetu za kidijitali, janga hili linaongezewa nguvu na kasi ya teknolojia,” amesema.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Ukatili wa kidijitali ni ukatili halisi. Hakuna visingizio kwa ukatili mtandaoni” ikilenga ongezeko la unyanyasaji wa mtandaoni, picha na video zinazobadilishwa au deepfakes, na kauli za chuki zinazowalenga wanawake.
Kwa mujibu wa ujumbe huo, “maudhui ya chuki dhidi ya wanawake yanatoka pembezoni na kuingia kwenye mkondo mkuu,” na hivyo kuongeza hatari za uhalisia kwani mashambulizi ya mtandaoni mara nyingi huishia kuwa madhara ya kimwili, ikiwemo ufuatiliaji, dhuluma, na hata mauaji ya wanawake kwa misingi ya kijinsia.
Serikali na kampuni za teknolojia zatakiwa kuchukua hatua
Akiliita jangga hili kuwa haukubaliki, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka serikali kutunga sheria zinazoharamisha ukatili wa kidijitali na kuimarisha huduma za msaada kwa waathiriwa.
“Kumaliza janga hili kunahitaji hatua kutoka kwetu sote,” amesisitiza.
Ameyashinikiza pia makampuni ya teknolojia kubeba wajibu zaidi akisema
“Kampuni za teknolojia lazima zihakikishe kuwa majukwaa yao ni salama na yanawajibika.”
Ujumbe huo umeitaka jamii na makundi ya kijamii kuungana katika “msimamo wa kutovumilia kabisa chuki mtandaoni.”
Wito wa umoja miaka 30 ya Azimio la Beijing
Dunia inapoadhimisha miaka 30 tangu Azimio muhimu la Beijing la mwaka 1995 kuhusu haki za wanawake, Katibu Mkuu ametoa wito wa kujitolea upya kwa pamoja.
“Katika maadhimisho ya miaka 30 ya Azimio la Beijing, naiomba dunia iungane kukomesha ukatili dhidi ya wanawake popote pale,” amesema. “Pamoja, tunaweza kujenga dunia isiyo na hofu ambako kila mwanamke na kila msichana anaweza kushamiri.”
Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Novemba na ndiyo ufunguzi wa Siku 16 za Kampeni dhidi ya Ukatili wa Kijinsia duniani kote.