Ripoti hiyo, “Maendeleo katika Uchumi wa Eneo la Palestina Linalokaliwa kwa Mabavu,” inabaini kwamba miaka miwili ya ongezeko la operesheni za kijeshi na vizuizi imechochea “anguko lisilokuwa na kifani katika uchumi wa Palestina,” likitokana na mazingira ya muda mrefu ya udhaifu wa kiuchumi na taasisi.
“Mwisho wa mwaka 2024, Pato la Taifa yaani GDP la Palestina lilirejea katika viwango vya mwaka 2010, huku pato la kila mtu likirudi katika kiwango cha mwaka 2003,” imesema UNCTAD, ikisisitiza kuwa “miaka 22 ya maendeleo imefutika kwa muda usiofikia miaka miwili.”
Watoto wameketi kati ya vifusi vya nyumba za familia zao zilizoharibiwa katika Jiji la Gaza, kuonyesha ukubwa wa uharibifu katika eneo hilo.
Miundombinu yaharibiwa, janga la kijamii laongezeka
UNCTAD inaripoti uharibifu mkubwa wa miundombinu, rasilimali za uzalishaji na huduma za umma, hali iliyorudisha nyuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa miongo kadhaa.
Mgogoro unaotokana na uharibifu huo sasa unachukuliwa kuwa miongoni mwa madhara makubwa kumi ya kiuchumi duniani tangu mwaka 1960.
“Kiwango cha uharibifu na usumbufu hakijawahi kushuhudiwa,” amesema mchumi mmoja wa UNCTAD aliyeshiriki katika tathmini hiyo. “Kila sekta kiuchumi, kijamii, kibinadamu na kimazingira imevutwa katika mgogoro kwa wakati mmoja.”
Hali katika Ukanda wa Gaza ni mbaya zaidi. Ripoti hiyo inasema kwamba eneo hilo linapitia “mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kurekodiwa popote,” huku idadi yote ya watu wakitumbukia katika umaskini wa kila aina.
Kuporomoka kwa mapato na ukosefu wa fedha
Uharibifu wa kiuchumi unazidishwa na kushuka kwa mapato ya Serikali ya Palestina. Ripoti hiyo inaonesha kuwa fedha za makusanyo ambazo hukusanywa na Israel kwa niaba ya Serikali ya Palestina zimezuiliwa, huku mapato ya ndani yakipungua kwa kasi kufuatia mgogoro huo.
Hali hii imeiacha Serikali ya Palestina ikiwa na uwezo mdogo sana wa kuendelea kutoa huduma muhimu au kuwekeza katika ujenzi upya.
“Wakati ambao matumizi makubwa yanahitajika sana ili kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa, shinikizo la kifedha lipo kwenye kiwango chake cha juu zaidi,” UNCTAD imesema. “Uwezo wa Serikali kufanya kazi umeathiriwa vibaya.”
Mwanamke na watoto wawili wanatembea karibu na jiji la Jenin katika Ukingo wa Magharibi.
Ukingo wa Magharibi wakabiliwa na mdororo mbaya zaidi
Wakati anguko la Gaza likivutia uangalizi mkubwa, ripoti hiyo inaonesha kwamba Ukingo wa Magharibi pia unakabiliwa na mdororo wake mbaya zaidi wa kiuchumi.
UNCTAD inahusisha hali hiyo na ongezeko la kutokuwepo kwa usalama, vizuizi vya harakati na ufikiaji, pamoja na kupotea kwa nafasi za uzalishaji katika sekta zote.
“Machafuko yameusukuma uchumi wa Palestina kutoka hali ya kudumaa kwa muda mrefu hadi kufikia karibu anguko kamili,” ripoti hiyo inasema. “Athari zake ni kubwa na pana.”
UNCTAD inasema kwamba kurejesha uchumi huo kutahitaji msaada mkubwa na wa haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kwa upande wa kifedha na kisiasa.
“Kiwango cha hasara ni kikubwa sana, lakini kufufua uchumi bado kunawezekana endapo hatua madhubuti zitachukuliwa sasa,” amesema msemaji wa UNCTAD. “Huu ni wakati muhimu kwa watu wa Palestina na kwa uthabiti wa eneo zima.”