Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wanaingia siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wao wa kilele unaofanyika mjini Luanda, nchini Angola.
Umoja wa Afrika umetowa mwito wa kuweko ushirikiano imara wa kiuchumi na uwekezaji wa kiviwanda ndani ya bara hilo, huku Ulaya ikihimiza kwamba ushirikiano wa mabara hayo mawili ni muhimu hivi sasa kuliko wakati mwingine.
Kikao cha kwanza jana cha mkutano wa Luanda kimetowa fursa kwa pande zote mbili kujadili hatua za kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, huku wachambuzi wakisema ni hatua muhimu ambayo inahitajika ikiwa Ulaya inataka kuendelea kushikilia dhima yake kama mshirika wa juu wa bara hilo la Afrika.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen kwenye hotuba yake ya ufunguzi ameweka wazi kwamba maendeleo ya Ulaya na Afrika yanafungamana zaidi katika kipindi hiki kuliko wakati mwingine, akitambuwa kwamba pande zote zinahitaji kujenga ulimwengu wa kesho wa viwanda na kutia juhudi kubwa kuondokana na utegemezi unaoweza kusababisha hatari.
Vita ya kuwania ushawishi wa maslahi Afrika
Bara la Afrika limegeuzwa kuwa uwanja wa mapambano ya kuwania rasilimali muhimu za madini na nishati huku China, Marekani na Urusi zikiwemo katika utafutaji wa fursa hiyo ya kuimarisha zaidi mahusiano na bara hilo kama zilivyopia nchi za Ghuba na Uturuki.
Na bara la Afrika linatambuwa ukweli huo na ndio sababu kwenye mkutano wa Luanda, Rais wa Angola ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Joao Lorenzo kwenye hotuba yake ya ufunguzi amesema waziwazi kwamba huu ni muda wa kuondowa hali ya mazowea.
”Ni kwa lengo la kuondokana na hali hii ya mazowea, ndio sababu nasisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa ushirikiano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, na kutowa mwito wa kujitolea hali na mali kuendelea kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi tunaoujenga. Na kwa makampuni ya Ulaya na wawekezaji kulitazama bara la Afrika kuwekeza kwenye sekta za viwanda na zile zinazokuza uchumi kwenye bara hilo na kujenga maslahi ya pamoja”
Umoja wa Ulaya ni muwekezaji mkubwa wa nje wa moja kwa moja kwenye bara la Afrika kama ambavyo pia ni mshirika wake wa kwanza wa kibiashara. Shughuli za kibiashara za bidhaa na huduma kati ya pande hizo mbili ziligonga yuro bilioni 467 mnamo mwaka 2023 kwa mujibu wa Brussels.
Wafuatiliaji karibu wa ushirikiano wa Afrika na Ulaya wanasema Ulaya inabidi iwekeze kwenye sekta ya miundo mbinu nishati na miradi ya viwanda itakayotowa ajira barani Afrika, na sio kuendeleza mazowea ya kutowa matamko matupu ya kuliunga mkono bara hilo.
Msemaji wa Umoja wa Afrika Nuur Mohamud Sheekh anasema Afrika haitaki tu kupewa maazimio mapya bali inategemea ahadi za kweli za utekelezaji.
Mkutano huo ambao kauli mbiu yake ni kuunga mkono amani na maendeleo yenye ufanisi, utajadili pia hali ya migogoro inayoendelea.
Rais Lorenzo ameshagusia kuhusu hali ya usalama duniani inayozidi, akitaja migogoro ya Ulaya, Afrika hadi Mashariki ya Kati.