
Taarifa hiyo inaonesha kuwa uchambuzi wa kisayansi na kiutendaji unathibitisha kukomeshwa kwa mfuatano wa maambukizi.
“Kwa niaba ya serikali na tukizingatia viashiria vyote vya kisayansi na kiutendaji vinavyothibitisha kuwa mfuatano wa maambukizi ya virusi umekatizwa ninatangaza rasmi mwisho wa mlipuko wa 16 wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” amesema Dkt. Samuel Roger Kamba, Waziri wa Afya ya Umma, Usafi na Ustawi wa Jamii.
Hatua za haraka na za uratibu mzuri ulioratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO na wadau wengine umekuwa muhimu katika kudhibiti ueneaji wa virusi vilivyoathiri eneo la Afya la Bulape, jamii ya vijijini iliyo na miundombinu duni ya barabara na mawasiliano.
Kwa ujumla, kulikuwa na visa 64 ambapo 53 ni vilivyothibitishwa, 11 vinavyodhaniwa na vifo 45.
Hatua zilizochukuliwa
Jumla ya wataalam 112 wa WHO na wahudumu wa mstari wa mbele walitumwa kusaidia mamlaka za kitaifa kuongeza na kuendeleza juhudi za kukabiliana na mlipuko, na zaidi ya tani 150 za vifaa na mahitaji ya kitabibu ziliwasilishwa ili kulinda wahudumu wa afya na jamii.
“Kudhibiti na kumaliza mlipuko huu wa Ebola ndani ya miezi mitatu ni mafanikio makubwa. Mamlaka za kitaifa, wahudumu wa afya wa mstari wa mbele, washirika na jamii walichukua hatua kwa kasi na kwa umoja katika moja ya maeneo magumu kufikika nchini,” amesema Dkt. Mohamed Janabi, Mkurugenzi wa Kanda wa WHO barani Afrika.
Ameongeza kuwa “WHO inajivunia kusaidia hatua hizi na kuacha mifumo iliyoimarishwa, kuanzia maji safi hadi huduma salama, ambayo itaendelea kulinda jamii hata baada ya mlipuko kuisha.”
Kwa mara ya kwanza katika mlipuko, kituo cha ubunifu cha matibabu kijulikanacho kama Infectious Disease Treatment Module (IDTM) kilianzishwa ili kuboresha utoaji wa huduma salama na rafiki kwa mgonjwa.
Kituo hiki kilichotengenezwa na WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula Duniani (WFP) na wadau wengine kilibuniwa ili kulinda wahudumu wa afya kwa ufanisi zaidi huku kikiwezesha utoaji wa huduma bora na yenye heshima kwa wagonjwa.
Utoaji wa chanjo
Ili kulinda jamii na wahudumu wa afya, zaidi ya watu 47,500 walipatiwa chanjo dhidi ya Ebola, chanjo ikianza kutolewa kwa watu waliokuwa karibu na wenye maambukizi yaliyothibitishwa na baadaye kupanuliwa kwa jamii za ndani na jirani za Bulape.
Gavi, ambao ni Muungano wa chanjo Duniani , imecheza jukumu muhimu kwa kuwezesha utoaji wa haraka wa zaidi ya dozi 48,000 kutoka kwenye hifadhi ya chanjo ya kimataifa inayofadhiliwa na Gavi.
Msaada huo umewezesha pia kundi la kimataifa la kuwezesha utoaji chanjo kuweka dozi kabla ya matumizi nchini na, kwa ushirikiano na WHO na Wizara ya Afya, kutoa ufadhili wa utoaji chanjo, shughuli za usafirishaji na miundombinu ya baridi inayohitajika.
“Hatua za haraka kwa mlipuko huu wa Ebola ni ushahidi wa kujitolea kwa wahudumu wa afya, Wizara ya Afya, washirika na jamii na kile kinachowezekana pale taratibu za kukabiliana na magonjwa hatari yanayozuilika kwa chanjo zinapokuwepo,” amesema Allyson Russell, Meneja Mwandamizi wa Mpango na Usalama wa Afya Duniani katika muungano wa Gavi.
Allyson Russell anaeleza kuwa chanjo kutoka hifadhi ya kimataifa ya Gavi na utoaji wa haraka, pamoja na hatua kama ufuatiliaji wa mawasiliano, kutenga wagonjwa na usimamizi wa kesi, vimewezesha DRC kudhibiti mlipuko wa Ebola kwa kasi na kupunguza visa na vifo.
Anaongeza kuwa Gavi itaendelea kusaidia kwa kudumisha hifadhi ya chanjo na kuimarisha chanjo za kinga kwa wahudumu wa afya katika maeneo hatarishi.
Changamoto zilizojitokeza
Kwa mujibu wa WHO changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa maji safi katika hospitali ya Bulape. WHO na wadau waliweka mfumo wa mabomba ya maji hospitalini na kwa jamii, utakaotoa huduma kwa miaka ijayo. Aidha, ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya unaendelea ili kuimarisha mfumo wa afya kwa muda mrefu.
Mlipuko huo ulikuwa wa 16 nchini DRC tangu ugonjwa huo kugunduliwa mwaka 1976. Milipuko ya awali katika Jimbo la Kasai ilitokea mwaka 2007 na 2008.
Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari, unaoenea kwa kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mgonjwa au maito, au kupitia vitu vilivyochafuliwa na majimaji hayo.
Baada ya kutangazwa kumalizika kwa mlipuko huo, ufuatiliaji unahamia kwenye mfumo mpana wa IDSR. WHO inaendelea kushirikiana na mamlaka kuweka uangalizi na utayari wa hatua za haraka iwapo ugonjwa utarejea.
WHO inasema nchi hiyo sasa inaanza kipindi cha siku 90 za ufuatiliaji ulioboreshwa wa magonjwa. Kama sehemu ya uangalizi endelevu, programu ya malezi ya manusura iliyoanzishwa kwa msaada wa WHO na wadau wake inasaidia kutoa huduma jumuishi za baada ya kupona kwa manusura wa Ebola.