Makumi ya maelfu ya watu huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa, wametoa kauli mbiu “Muqawama; kutoka Paris hadi Palestina; wakiunga mkono Wapalestina.

Katika Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, mitaa ya Paris ilishuhudia moja ya maandamano makubwa ya mshikamano na watu wa Palestina. 

Jumamosi Novemba 29 wanaharakati na watu wa kawaida katika pembe mbalimbali za dunia, waliadhimisha Siku ya Kimataiifa ya Mshikamano na Wapalestina kwa maandamano, kampeni za upashaji habari, na wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti ili kukomesha ukaliaji kwa mabavu ardhi ya Palestina unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa uungaji mkono wa Magharibi ikiongozwa na Marekani.

Kutoka mzunguko wa Jamhuri hadi medani ya Taifa, makumi ya maelfu ya waandamanaji, wakiwa wameshikilia bendera za Palestina na mabango yenye kaulimbiu kama vile “Komesha mauaji ya kimbari,” “Gaza, Paris iko pamoja nawe,” na “Palestina lazima ikombolewe,” walipaza sauti zao za hasira dhidi ya Israel na huruma kwa Wapalestina na kuwafikishia ujumbe huo walimwengu.

Maandamano hayo yalikuwa ni mwitikio kwa kile waandamanaji wanachokiita “kutwisha mpango ghushi wa amani wa Marekani na Israel” na “kinga kamili” kwa uhalifu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Maandamano hayo, yaliyoitishwa na zaidi ya asasi za kiraia (NGOs) 80, vyama vya mrengo wa kushoto na vyama vya wafanyakazi, yalihudhuriwa na mchanganyiko wa raia, wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa kama vile Jean-Luc Mélenchon. Maandamano ya Paris yalikuwa ishara ya wazi ya mgawanyiko mkubwa kati ya jamii ya Ufaransa na serikali ya Rais Macron, ambayo inabaki kuwa ya kuchukua tahadhari na inayounga mkono Tel Aviv.

Waandamanaji walikuwa na mabango yaliyosomeka: “Palestina, hatutanyamaza” na “Komesheni mauaji ya halaiki” – kaulimbiu ambazo zina sauti ndogo katika vyombo vya habari lakini zna mwangwi katika mitaa ya Paris.

Le Figaro, Libération, Omentier na France 24 ziliripoti kuwa, hasira ya waandamanaji haikuishia tu kwenye mashambulio ya mabomu ya miezi iliyopita; bali walilaani pia mauaji ya Wapalestina 322 tangu kusitishwa vita huuko Gaza Oktoba mwaka huu, kuharakisha ujenzi wa makazi, ghasia zisizo na kifani za walowezi na mauaji mengine.

Kuna video ziliozenea katika mitandao ya kijamii zikionyesha watu wawili wasio na ulinzi wakiwa wameinua mikono yao juu, na sekunde chache baadaye miili yao isiyo na uhai inaanguka chini.

Umoja wa Mataifa umeitaja hatua hiyo kuwa “mauaji ya pupa” na kutaka uchunguzi ufanyike, lakini serikali za Ulaya bado zinafadhalisha kuchukua mkondo usioeleweka wa “nasaha na kutoa tu kauli za kuonyesha wasiwasi.”

 “Wiki saba zimepita tangu kusitishwa mapigano, lakini hakuna kilichotatuliwa,” Anne Touyon, Mkuu wa Jumuiya ya Mshikamano wa Ufaransa na Palestina, aliiambia AFP. Alionya kwamba ujenzi wa makazi ulikuwa ukiendelea kwa kasi “ya ajabu” na kwamba vurugu za walowezi katika Ukingo wa Magharibi zimefikia hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Mkuu wa Jumuiya ya Mshikamano wa Ufaransa na Palestina aliongeza: “Vikwazo ni muhimu; ndiyo njia pekee ya kuilazimisha Israel kuheshimu sheria za kimataifa.” Lakini kuna masikio ya kusikia haya?

Hili ndilo swali ambalo lilisikika wakati wote wa maandamano. “Binadamu wote wanatazama na hawawezi kufanya lolote,” alisema mwanamke mwenye umri wa miaka 72 akiwa amesimama kwenye umati wa watu akiwa na bendera ya Palestina. Kauli hii inachora picha kamili ya mgogoro wa kimaadili wa nchi za Magharibi.

Nchi za Magharibi zinatumia mabilioni ya dola katika vita vinavyoitwa “vya kibinadamu”, lakini zinajificha nyuma ya kuta za uhalali wa kisiasa katika kukabiliana na vifo vya maelfu ya watoto huko Gaza.

Maandamano ya kuunga mkono Palestina

“Mauaji ya halaiki yanaendelea,” alisema Bertrand, fundi mwenye umri wa miaka 42 ambaye alishiriki katika maandamano hayo. Alikumbusha kwamba bila vikwazo vya kiuchumi na kisiasa, zana pekee zilizobaki ni “mashinikizo ya barabarani” na “kilio cha mashirika ya kiraia.”

Vyama vya wafanyakazi na mashirika ya kiraia kama vile Amnesty International, Attac, na Cimade pia vilijiunga na maandamano hayo, kuonyesha kwamba suala la Palestina nchini Ufaransa sio tena takwa la kando au la mrengo wa kushoto, bali ni daghadagha na wasiwasi wa umma na mpasuko mkubwa wa kisiasa; pengo kati ya raia wanaotaka kuheshimiwa kanuni za haki za binadamu, na serikali ambayo imegawanyika kati ya “kuunga mkono Israel” na “kudai kutoegemea upande wowote.”

Katika mazingira haya, kimya cha serikali ya Ufaransa na kutochukua hatua kwa Umoja wa Ulaya kumechochea hasira za waandamanaji. Wanauliza inawezekanaje kwa Ulaya kutekeleza haraka vikwazo na mifumo ya mashinikizo dhidi ya Russia lakini inaridhika na taarifa zisizo na tija dhidi ya Israel, ambayo inakiuka sio tu sheria za kimataifa lakini pia kanuni za kimaadili?

Kaulimbiu “Watoto wetu hawatakuwa wanajeshi wa Macron,” “Ondoeni mzingiro,” na “Palestina lazima ikombolewe” hazikuwa tu nara za maandamano, lakini ishara kwamba watu wa Ufaransa hawako tayari kunyamaza mbele ya sera za kupuuza na kutojali maisha ya wanadamu.

Kwa hakikka maandamano haya, yalikuwa kioo kwa Ulaya, kioo ambacho kilionyesha sura mbaya ya nafasi ya kutochukua hatua, ukimya wa kimkakati, na hofu ya kuikosoa Israel kwa bara ambalo linadai kuwa kinara wa maadili ya ulimwengu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *