Kampuni ya META inayomiliki mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp, imefunga akaunti za wanaharakati kadhaa wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania, hatua iliyoibua maswali kuhusu Serikali ya Tanzania kuingia uhuru wa maoni ya raia wake.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Miongoni mwa akaunti za wanaharakati mashuhuri zilizofungwa na ambazo zilikuwa na idadi kubwa ya wafuasi ni Pamoja na ile ya Instagram ya mwanaharakati anayeishi Marekani Mange Kimambi na Maria Sarungi aliyeko Kenya.
Kupitia akaunti zao za X inayomilikiwa na Tajiri Elon Musk, Mange Kimambi na Maria Sarungi, walichapisha screenshot za ujumbe waliopokea kutoka Meta kuwataarifu kuzuia na kuzifunga kabisa akaunti zao za Instagram na WhatsApp.

Wanaharakati hao Pamoja na wenzao wengine ambao pia akaunti zao zimezuiwa na Meta, wamekashifu uamuzi wa kampuni hiyo, wakiituhumu kushirikiana na serikali ya Tanzania, kuminya uhuru wa watu kutoa maoni na raia kuokea taarifa kuhusu yanayotokea nchini mwao.
Kufungwa kwa akunti hizi kumekuja siku chache kupita tangu Serikali ya Tanzania iahidi kuanza kuwachukulia hatua wanaharakati inaowatuhumu kuwa walichochea machafuko ya Octoba 29, ambapi tayari Mange kimambi amefunguliwa mashtaka ya utakatishaji fedha.

Haya yanajiri wakati huu Serikali ikiwaonya wanaharakati na raia wanaochochea vurugu zaidi, hasa wakati huu kukiwa na taarifa za mpango wa maandamano mengine Desemba 9.
Katika hatua nyingine, RFI Kiswahili imezungumza na wanaharakati kadhaa walioko Tanzania na nje ya Tanzania ambao wamesema wanahofia usalama wao kutokana na kufuatiliwa na Idara za usalama, baadhi wakiomba kutotoa maoni kuhusu yanayoendelea.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, ikiwemo umoja wa Mataifa, wamesisitiza kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu vurugu za Octoba 29 ambapo mamia ya raia waliuawa na kujeruhiwa, huku pia wakitoa wito kwa serikali kulinda haki za binadamu ikiwemo uhuru wakuandamana na maoni.