Kama mwanzilishi wa shirika la Footprint to Freedom, linaloongozwa linalolenga kuwawezesha na kuwarejesha katika jamii waathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu, anatetea kuhakikisha sauti za manusura zinakuwa kiini cha utungaji wa sera na hatua za serikali duniani. 

Katika mazungumzo na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, akiwa jijini New York, Marekani, Bi. Oringo anatafakari safari yake binafsi jinsi alivyokabiliana na mshtuko, kurejesha sauti yake, na kuendelea kuleta mabadiliko kupitia utetezi wake usiokoma.

Anaeleza kwamba usafirishaji haramu wa binadamu ni matokeo ya miaka ya mazingira hatarishi ambayo hayajapewa rasilimali za kutosha, hayajafanyiwa utafiti wa kutosha, na pia kuongezwa ukali na athari za mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama, na ukosefu wa elimu.

Mwanamke huyu wa nchini Uganda, takribani miaka 17 iliyopita akiwa na umri mdogo tu wa miaka 15 mama yake alifariki na hivyo akaenda katika kambi ya wakimbizi wa ndani kumtafuta mmoja wa ndugu zao na huko ndiko alikutana na mtu kutoka barani Ulaya aliyemhakikishia kumsaidia kumpeleka nje ya nchi kumlea na kumpa elimu.

Malaika Oringo anaeleza akisema, “kwangu mimi, ilikuwa ni matamanio ya kwenda shule, na mfanyabiashara alitumia udhaifu huo. Niliahidiwa maisha bora na kupata elimu ya bure, lakini badala yake niliishia kuuzwa na kunyanyaswa nikiwa na umri wa miaka kumi na sita barani Ulaya.”

Mwanaume huyo aliyemchukua alimuuza mara tu baada ya kutua katika Uwanja wa ndege nchini Luxembourg na waliomnunua walimsafirisha kwa njia ya barabara hadi Amsterdam, Uholanzi

Hata baada ya muda mrefu wa kunyanyaswa, alipofanikiwa kupata usaidizi wa kisheria, kesi haikwenda mbali kwani kutokana na muda mfupi wanaopewa manusura kama yeye na kutokusikilizwa kwa kina, “walishindwa kumpata mfanyabiashara aliyenipeleka.

Duniani kote, sheria za kupambana na usafirishaji wa binadamu zinahusisha uhalali wa uathirika na uchunguzi unaoendelea. Hivyo uchunguzi unapokamilika, haki ya kupata huduma, elimu, na matibabu huondolewa, aanasema, “kwangu, huduma hizo zilisitishwa, nikabaki bila nyaraka kwa zaidi ya miaka kumi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *