“Afghanistan inaweza kurejea kikamilifu tu baada ya mamlaka zisizo rasmi kutimiza wajibu wao wa kimataifa,” amesema Georgette Gagnon, Mwakilishi Msaidizi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan na Mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA.
“Mamlaka zisizo rasmi za Taliban zinaendelea kukosa au kupuuza fursa za mazungumzo ya kimataifa na jumuiya ya kimataifa.”
Mwanamke akiwachemshia maji watoto wake sita nje ya nyumba yake iliyoharibika kufuatia mafuriko katika Mkoa wa Baghlan kaskazini mwa Afghanistan.
Kutengwa kwa wasichana kwenye kila sekta ya umma
Gagnon akiwakilisha taarifa bele ya wajumbe wa Baraza hilo la Usaama amelaani kutengwa kwa kina kwa wasichana nchini Afghanistan kutoka karibu kila kipengele cha maisha ya umma nchini humo.
Amesisitiza kuwa Waafghanistan wote, wanaume na wanawake, wanakumbwa na ukiukwaji wa haki zao za msingi kutokana na utekelezaji wa sheria ya “Uendelevu wa Maadili na Kuzuia Uovu” ya Taliban.
“Kuzorota kwa haki za binadamu siyo shida pekee,” Gagnon amesema, akionesha athari zinazojumuisha matatizo ya kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, na dharura za kibinadamu, huku zikichangiwa na kurrejea kwa karibu Waafghanistan milioni 2.5 kutoka Iran na Pakistan.
Amebainisha mgawanyiko mkubwa ndani ya Taliban: “Kundi moja linataka kuitenga Afghanistan kutoka katika ulimwengu, wakati lingine linaelewa kuwa nchi haiwezi kuishi bila uhusiano wa kimataifa.”
Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Afghanistan.
Dhuluma za kibinadamu zimefurutu ada- Fletcher
Tom Fletcher, Msaidizi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na msaada wa Dharura wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa karibu Waafghanistan milioni 22 watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka 2026, idadi hiyo ikiwakilisha nafasi ya tatu duniani baada ya Sudan na Yemen.
“Ombi letu ni dola bilioni 1.7 kufikia watu milioni 17.5,” amesema Fletcher akiongeza kuwa “Lakini kushughulikia mahitaji muhimu ya zaidi ya watu milioni 3.9, inahitajika dola milioni 375.9 kama kipaumbele.”
Amesisitiza kiwango cha dharura kwamba Waafghanistan milioni 17.4 wanakabili njaa, vituo 422 vya afya na vituo 305 vya lishe vimefungwa, na kuacha watu milioni 3 bila huduma za afya na watoto 1.1 milioni bila huduma muhimu.
Fletcher pia ametaja kurudi kwa wakimbizi, matetemeko mawili makubwa ya ardhi, na ukame unaowaathiri watu milioni 3.4.
Upungufu wa fedha na vikwazo dhidi ya wanawake wahudumu wa kibinadamu wa Afghanistan vinasababisha changamoto kubwa kwenye utoaji msaada. “Tunawahitaji. Afghanistan inawahitaji,” Fletcher amesisitiza, akihimiza Taliban kuondoa vizuizi hivi.
Negina Yari, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Window for Hope, akitoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Afghanistan.
Wanaharakati walaani kufutwa kwa haki za wanawake
Negina Yari, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa “Dirisha la matumaini” au Window for Hope, amelitaka Baraza la Usalama kuwataka Taliban kuondoa vikwazo vyote vilivyowekwa kwa wanawake.
“Kihalisi, karibu haki zote za wanawake wa Afghanistan za kujifunza, kufanya kazi, na kushiriki katika maisha ya umma na kisiasa zimesambaratishwa kwa muundo wa kimfumo” amesema Yari akiongeza kuwa “Wamepunguzwa kuwa wapokeaji tu wa misaada badala ya kuwa washiriki hai wa maisha yao.”
Yari ameonya kuwa vizuizi vinavyoongezwa kwa wahudumu wanawake wa kibinadamu vinaweka hatarini operesheni zijazo za msaada na kuongeza kutengwa kwa wanawake.
Ametaka Umoja wa Mataifa kuhakikisha wanawake wa Afghanistan wanaweza kufanya kazi kwa usalama kwa Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na mashirika ya ndani, na kuwawekea wajibu viongozi wa Taliban kupitia vikwazo maalumu kwa ukiukaji mkubwa dhidi ya wanawake na wasichana.
Taarifa hii inaonesha janga kubwa linalokumba Afghanistan ukiukaji wa haki za binadamu, dharura za kibinadamu, na kutengwa kisiasa kutokana na utawala wa Taliban na kusisitiza wito wa jumuiya ya kimataifa juu ya uwajibikaji kabla ya kurejea kwa nchi hiyo.