Tuzo hiyo ya kimataifa, inayotolewa kila mwaka huko Geneva Iswisi, inawapa heshima wale wanaoonesha ujasiri wa hali ya juu, huruma isiyo na mipaka, na kujitolea kwa dhati katika kuwasaidia watu waliolazimika kukimbia makwao.
Washindi hawa wamechaguliwa kwa kulinda na kusaidia wakimbizi, watu waliokoseshwa makazi ndani ya nchi na wale wasio na utaifa, kupitia hatua zinazozidi wito wa wajibu na zinazobadili maisha ya wale wanaokumbana na changamoto kubwa za kibinadamu.
Kuhusu Tuzo ya Nansen
Kuanzishwa kwa Tuzo ya Nansen mwaka wa 1954, kunawapa heshima watu binafsi, makundi na mashirika yanayokwenda mbali zaidi ya wajibu wao katika kuwalinda wakimbizi, watu waliofurushwa kutoka kwenye makazi yao ndani ya nchi, pamoja na watu wasio na utaifa.
Taban Shoresh ni mfanyakazi wa misaada, mwanaharakati wa haki za wanawake na mwanzilishi wa The Lotus Flower, shirika linaloongozwa na wanawake ambalo linasaidia waathirika wa migogoro nchini Iraq.
Washindi wa mwaka wa 2025 ni pamoja na chifu wa kijiji nchini Cameroon aliyesaidia kuunganisha wakimbizi 36,000, mwanzilishi wa shule inayoendeshwa na wakimbizi nchini Tajikistan, shirika la wanawake nchini Iraq linalowafikia waathiriwa 105,000 wa mizozo, mwekezaji nchini Mexico aliyesaidia kutoa ajira kwa mamia ya wakimbizi, na wahudumu wa mstari wa mbele nchini Ukraine wanaobaki kuwahudumia watu hata wengine wanapoondolewa.
Kamishna Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi. wakati wa kutangaza washidi hao amesema
“Tuzo ya Nansen inasherehekea ujasiri na huruma isiyo ya kawaida, washindi wa mwaka huu wanatukumbusha kuwa hata nyakati za giza, huruma haizimiki. Uaminifu wao katika kuwalinda na kuinua hadhi ya watu waliokimbia makwao unatupa matumaini. Wanadhihirisha dhamira yaNansen ya imani kwamba kila mtu anayelazimika kukimbia anastahili utu, usalama na matumaini.”
Mshindi wa jumla wa tuzo hiyo
Mshindi wa kimataifa wa mwaka huu, Chifu Martin Azia Sodea kutoka Cameroon, ni kiongozi mbunifu ambaye amegusa maisha ya maelfu ya watu kwa ubinadamu wake.
Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, walipowasili kijijini kwao, watu wa Gado-Badzéré hawakuwafukuza. Wakiongozwa na Chifu Sodea na familia yake, waliwapa wageni hao ardhi ya makazi na kilimo ili wapate kuanza upya. Uongozi wake umeibadilisha jamii ndogo kuwa mfano wa mshikamano, ikiongozwa na imani kwamba wanaowasili wakiwa katika shida wanastahili msaada.
Chifu Sodea pia amewahamasisha viongozi wengine wa jadi kuwasaidia wakimbizi, na hivyo kuchochea mabadiliko ya mtazamo kuhusu jinsi wakimbizi wanavyokaribishwa katika eneo hilo.
Ujumbe wake ni rahisi lakini wenye uzito: “Sisi sote ni binadamu, na tunapaswa kusaidiana.”
Chifu Sodea ameongeza kuwa “Tunapaswa kuanza kwa kushughulikia mahitaji ya kijamii. Ndiyo mtazamo huu wa kijamii uliowaokoa watu hawa, kwa sababu baadhi walikuwa wanakufa njiani wakija hapa. Ilibidi tujitoe, tuwapelekee chakula na tuwaokoe, hatungeweza kuwaona kaka zetu wakifa. Hakuna tofauti kati ya wakimbizi na wenyeji. Tunaishi pamoja.”
Pablo Moreno Cadena, kiongozi mwanabiashara nchini Mexico, amekuwa kielelezo cha kujumuishwa kwa wakimbizi nchini humo.
Washindi wa kanda kwa mwaka wa 2025 ni:
Pablo Moreno Cadena (Amerika) – kiongozi wa biashara nchini Mexico ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ujumuishaji wa wakimbizi nchini humo. Kama afisa mwandamizi katika MABE, kampuni kubwa ya utengenezaji wa vifaa vya nyumbani, amehamasisha kampuni kuajiri kwa uwazi na kuwaunganisha wakimbizi katika mfumo wa ajira yake
Proliska (Ulaya) – Shirika la Ukraine linalotoa misaada ya kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni 3.2, hata katika maeneo hatari zaidi. Baada ya mashambulizi ya anga, Proliska huwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika kuwasaidia walio hatarini.
Taban Shoresh (Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini) – Mhudumu wa misaada, mtetezi wa haki za wanawake na mwanzilishi wa The Lotus Flower, shirika linaloongozwa na wanawake linalosaidia waathiriwa wa migogoro nchini Iraq. Kama manusura wa mauaji ya kimbari, Taban ameamua kutumikia wanawake na wasichana waliokimbia makwao katika eneo la Kurdistan.
Negara Nazari (Asia-Pasifiki) – Mkimbizi kutoka Afghanistan na mwanzilishi mwenza wa Kituo cha Kujifunza cha Ariana nchini Tajikistan. Akiwa mhitimu wa udhamini wa DAFI katika masuala ya uchumi, Negara ameacha taaluma ya kampuni na kuchagua kuanzisha shule kwa ajili ya wanafunzi wa Afghanistan waliokosa fursa ya elimu.