
BEKI wa JKT Tanzania, David Bryson amekimwagia sifa kikosi cha timu hiyo kilichoanza kwa kasi kubwa msimu huu katika Ligi Kuu, huku akifichua kilichowabeba ni mbinu za kocha Ahmad Ally sambamba na wachezaji kutekeleza kila walichoelekezwa.
Brayson aliwahi kuichezea Yanga na KMC kabla ya kutua JKT Tanzania ambayo ameitumikia kwa misimu miwili sasa.
Beki huyo wa kushoto aliliambia Mwanaspoti, tangu atue JKT huu unaweza kuwa msimu bora zaidi kwake, kwani ameshuhudia timu ikicheza mechi kwa ubora wa hali ya juu.
Amesema, JKT ni timu ambayo inaongozwa na wachezaji wote wazawa na kwake anaona wameiwakilisha vyema bendera ya timu hiyo kwani hawajaanza msimu kinyonge.
“Hadi sasa ukiangalia mfungaji bora anatoka kwetu na kileleni tupo sisi, hilo ni jambo ambalo tutajivunia sana msimu huu na ni ishara nzuri kwetu,” amesema Brayson na kuongeza;
“Katika timu ambazo zinawapasua kichwa wapinzani JKT ni mojawapo kwa sasa. Hii ni heshima kubwa kwa wazawa ambao tunaichezea. Malengo yangu msimu huu hayako mbali na ya timu, kwanza nataka kuwa mmoja kati ya mabeki watakaokuwa bora na niweze kuisaidia klabu.
“Kweli mbinu za kocha zimetusaidia sana, sisi hatuchezi tu ila tunatumia akili kubwa ya kumsoma mpinzani.”
“Nidhamu na mbinu tunazopewa zinatupa matunda makubwa.”
Rekodi zinazidi kupandisha thamani ya beki huyo kwani katika mechi 10 amecheza tisa sawa na dakika 810, huku akikosa mchezo mmoja dhidi ya Simba.
JKT kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikicheza mechi 10 na kuvuna pointi 17, ikishinda mechi nne, sare tano na kupoteza mmoja, ikifuatiwa na watetezi Yanga wenye pointi 16 kupitia mechi sita sawa na Pamba Jiji iliyopo nafasi ya tatu.