UJIO wa kocha mkuu mpya, Steve Barker ndani ya Simba umewafanya mastaa wa timu hiyo kuanza kukuna vichwa kutokana na kuwaambia wazi kwamba hataangalia ukubwa wa majina ya wachezaji waliopo kikosini, isipokuwa watapimwa kwa ufanisi wao uwanjani na jinsi watakavyoibeba timu akianza na michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Kocha huyo aliyetambulishwa Desemba 19 mwaka jana ameanza rasmi kazi na kikosi hicho na kabla ya jana kuondoka jijini Dar es Salaam kwenda Zanzibar, inaelezwa alikutana na wachezaji na kuzungumza nao na baadhi ya wachezaji walizungumza na Mwanaspoti wamefichua kocha huyo amewaambia wazi kila mmoja apambane.
Kwa mujibu wa wachezaji hao walioomba kuhifadhiwa majina yao, wamesema kocha Barker amewataka waache kabisa mawazo ya majina makubwa au historia binafsi, akisisitiza kuanzia sasa kila mchezaji atalazimika kuthibitisha ubora wake kwa vitendo uwanjani.
Wachezaji hao wamesema kocha huyo amewataka kila mmoja aamini uwezo alionao, lakini zaidi apate matokeo kupitia juhudi, nidhamu na kujitoa kikamilifu uwanjani na wasitarajie kubebwa na majina waliyonayo.
Beki mmoja wa kikosi hicho amesema; “Kocha anataka tujiamini, lakini kila mmoja aonyeshe ubora na kuipigania Simba kwa kila hali na kwamba hakuna atakayepata nafasi kwa sababu ya jina.”
Aliongeza: “Kocha amekuwa wazi kuhusu matarajio ya mashabiki wa Simba, akisisitiza klabu ina mashabiki wengi wenye kiu ya mafanikio, hasa ubingwa, jambo linalotupa wajibu mkubwa wa kubadilisha matokeo ya timu.
“Bahati nzuri ametuambia wazi kuwa mashabiki wanataka ubingwa, uongozi nasi wachezaji tunataka pia. Ndio maana tupo hapa, tunatakiwa kukamilisha hilo.”
Naye mmoja wa viungo wa timu hiyo amesema kocha huyo anaonekana ni mkali kupitia mazungumzo yake, lakini ni mtu anayependa nidhamu na amewasisitiza kufanya kazi kwa bidii hataki kuona mchezaji yeyote akiridhika na kiwango chake.
“Ni kocha mzuri, anatusukuma, jinsi anavyozungumza ni ngumu kwani anaonekana ni mkali, lakini ujumbe wake uko wazi lazima tupambane kwa ajili ya Simba. Amesisitiza ushindani wa nafasi ndani ya kikosi, amesema kila mchezaji ana nafasi ya kucheza endapo ataonyesha kiwango bora, ujumbe huo umeongeza hamasa ya ushindani mzuri kambini.”
Kiungo amesema kwa muktadha huo ni kwamba kwa sasa kila kitu kinaanza upya Msimbazi.
Mchezaji mwingine alifichua kuwa, kocha amesema kipimo cha kwanza kwa wachezaji ni michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea Zanzibar, Simba ikipangwa Kundi B na Muembe Makumbi na Fufuni, huku ikiwa na rekodi ya kubeba taji hilo mara nne ikiwa nyuma ya Azam iliyotwaa mara tano ikiwa ndio kinara tangu 2007.
“Kocha ametaja mashindano ya Mapinduzi yanayofanyika Zanzibar kuwa ni kipimo muhimu cha kuona uwezo halisi wa wachezaji wote, akitutaka kwenda huko na kumuonyesha ubora tulionao. Ametuambia hapo ndipo mwanzo wa safari nzima ya Simba chini yake na ametutaka tupambane kumuonyesha kile tulichonacho.”