Dar es Salaam. Tangu ameanza mradi wa kuwasimamia wanamuziki wenzake chini ya WCB Wasafi, hakuna ubishi kuwa Diamond Platnumz amekuwa na athari chanya tena za moja kwa moja katika mafanikio ya wasanii wake.

Kuna mafanikio na rekodi nyingi katika Bongofleva ambazo zinapatikana kwa wasanii waliokuzwa kimuziki na WCB Wasafi pekee, na huwezi kuzungumzi hayo bila kulitajia jina la Diamond ambaye ndiye mwanzilishi.

Diamond aliyetoka kimuziki mwaka 2009 akishinda Tuzo ya Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010, wakati anaanza kupata mafanikio kimataifa ndipo alianza kusaini wasanii WCB Wasafi.

Mafanikio yake kimataifa yalikuja baada ya kumshirikisha staa wa Nigeria, Davido katika wimbo wake, My Number Remix (2013) uliofanya vizuri hadi kutajwa kuwania vipengele viwili tuzo za MTV MAMAs 2014.

Alianza kwa kumtambulisha Harmonize aliyetoka na wimbo wake, Aiyola (2015), na kuja kushinda tuzo ya AFRIMMA Marekani 2016 kama Msanii Bora Chipukizi baada ya kufanya hivyo kupitia AEAUSA 2016.

Baada ya Harmonize, WCB Wasafi iliwasaini wasanii wengine kama Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018), Zuchu (2020) na D Voice (2023).

Hadi sasa WCB Wasafi inasimama kama rekodi lebo yenye nguvu kubwa ya ushawishi hapa Afrika Mashariki ikisifika kwa kutengeneza majina makubwa yenye mafanikio katika kiwanda cha muziki.

Ni hivi karibuni msanii wake wa zamani, Mbosso ameweka rekodi kwa video zake kutazamwa zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao wa YouTube akiwa ni mwanamuziki wa tano kutokea Tanzania kufikia namba hizo.

Mbosso, mwanachama wa zamani wa kundi la Yamoto Band, kwa ujumla anaungana na Diamond, Rayvanny, Harmonize na Zuchu ambao walitangulia kuifikia rekodi hiyo ya kipekee na yenye heshima kubwa.  

Ukitazama orodha hiyo, utabaini wasanii wote wamepita WCB Wasafi au bado wapo ndani ya lebo, na hizo ndizo adhari chanya za Diamond kwa wasanii anaowasimamia ingawa baadhi baadaye humgeuka.

Ikumbukwe kuwa Diamond, mshindi wa tuzo za MTV EMAs mara tatu, ndiye mwanamuziki wa kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kutazamwa zaidi ya mara bilioni 1 YouTube, rekodi aliyoiweka hapo Juni 2020.

Kwa Tanzania, baada ya Diamond aliyefuatia kuweka rekodi kama hiyo ni Rayvanny hapo Oktoba 2023, kisha Harmonize – Novemba 2023, Zuchu – Novemba 2025 na Mbosso – Desemba – 2025.  

Hata hivyo, Rayvanny, Harmonize na Mbosso, wamefikia rekodi hiyo wakiwa tayari wameachana na WCB Wasafi, ni Zuchu pekee ambaye rekodi hiyo imemkuta bado yupo ndani ya lebo.  

Kwa Zuchu mafanikio hayo yanakuja takribani mwaka mmoja tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024) yenye nyimbo 13 na kuwashirikisha wasanii saba kutokea Bongo na kimataifa.

Nyimbo zake kama Sukari (2021), Kwikwi (2022), Honey (2023), Nyumba Ndogo (2021) na Cheche (2020), zimechangia kwa sehemu kubwa kwa yeye kufikisha hizo ‘views’ bilioni 1 YouTube.

Mathalani, mnamo Desemba 2021, video ya wimbo wake ‘Sukari’ iliandika rekodi kama video ya muziki iliyotazamwa zaidi YouTube barani Afrika kwa mwaka huo ikitazamwa zaidi ya mara milioni 60.

Baadaye ilikuja kuweka rekodi kama video ya kwanza kutoka kwa msanii solo nchini Tanzania na Afrika Mashariki kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikifanya hivyo hapo Machi 2024.

Mbali na Sukari (2021) yake Zuchu, nyingine ni Kwangwaru (2018) yake Harmonize, Number One (2020) yake Rayvanny, na Enjoy (2023) yake Jux akimshirikisha Diamond.
Kwa upande wake Diamond, ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki ambaye ana video nyingi zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube.

Diamond, mshindi wa TMA zaidi ya mara 20, anazo video tano zenye namba hizo ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Nana (2015) na Jeje (2020) ambao ni wimbo wake wa kwanza solo kufanya hivyo.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *