Akizungumzia tukio la kukamatwa kwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, lililofanywa na Marekani tarehe 03 Januari 2026, Kamishna Türk amesisitiza tena wasiwasi wake mkubwa kwamba operesheni hiyo ya kijeshi imekiuka misingi ya ulinzi wa nchi huru.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi, msemaji wa Kamishna Mkuu, Ravina Shamdasani, ameeleza hatua hiyo ya Marekani imefanya “mataifa yote duniani kuwa katika hatari zaidi.”
Shamdasani amepinga hoja ya Marekani iliyojaribu kuhalalisha jeshi lake kumchukua Rais wa Venezuela ya kuwa nchi hiyo imekuwa na rekodi ya “muda mrefu na ya kutisha” ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na serikali ya Venezuela.
Alisisitiza kuwa: “Uwajibikaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu hauwezi kupatikana kupitia uingiliaji wa kijeshi wa upande mmoja unaokiuka sheria za kimataifa.”
Aliongeza kuwa, badala ya kuwa ushindi kwa haki za binadamu, uingiliaji huo wa kijeshi unaokiuka mamlaka ya Venezuela na Chata ya Umoja wa Mataifa, “unahujumu muundo wa usalama wa kimataifa,” jambo ambalo pia limeelezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Shamdasani ameeleza kuwa operesheni hiyo ya kijeshi inakiuka kanuni ya msingi ya sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaosema kuwa nchi hazipaswi kutishia wala kutumia nguvu dhidi ya uhuru wa kisiasa au mipaka ya nchi nyingine.
Haki zimekiukwa kwa muda mrefu
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ilifukuzwa kutoka Venezuela Februari 2024, kufuatia ripoti zake za mara kwa mara kuhusu kuzorota kwa hali ya haki za binadamu nchini humo. Uchunguzi huru ulioagizwa na Baraza la Haki za Binadamu pia umebainisha ukiukwaji mkubwa na unaoendelea dhidi ya wapinzani wa serikali.
“Wananchi wa Venezuela wanastahili uwajibikaji unaopatikana kupitia mchakato wa haki, unaozingatia waathirika,” alisema Shamdasani, akiongeza kuwa haki za wananchi hao “zimekiukwa kwa muda mrefu sana.”
Ameonya kuwa kukosekana kwa utulivu na kuongezeka kwa matumizi ya nguvu za kijeshi kufuatia uingiliaji wa Marekani kunaweza kuzidisha hali mbaya zaidi.
Shamdasani amebainisha kuwa hali ya hatari ilitangazwa Jumamosi ( tarehe 03 Januari 2026), hali iliyopelekea kuzuiwa kwa uhuru wa kutembea, kunyang’anywa mali kwa ajili ya ulinzi wa taifa, pamoja na kusimamishwa kwa haki ya kukusanyika na kuandamana.
“Tuna wasiwasi mkubwa, hasa kutokana na historia ya serikali ya Venezuela ya kukandamiza uhuru wa kujieleza, maandamano na mikusanyiko kwa kisingizio cha usalama wa taifa,” alisema.
Kamishna Mkuu ametoa wito kwa Marekani, mamlaka za Venezuela na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kunaheshimiwa kikamilifu sheria za kimataifa, ikiwemo haki za binadamu. Amesisitiza tena kuwa mustakabali wa Venezuela “lazima uamuliwe na wananchi wake pekee, kwa kuheshimu kikamilifu haki zao za binadamu, ikiwemo haki ya kujitawala na mamlaka juu ya maisha na rasilimali zao.”
Haki ipoje Venezuela?
Familia moja ya Venezuela inafunga safari ndefu na hatarishi kutoka mpaka wa kusini wa Peru hadi Lima.
Mtu mmoja moja kati ya wanne anahitaji msaada wa kibinadamu
Mbali na mgogoro wa kisiasa, karibu watu milioni nane — sawa na mtu mmoja kati ya wanne nchini Venezuela — wanahitaji msaada wa kibinadamu, kufuatia miaka ya kudorora kwa uchumi, vikwazo, ukandamizaji na kutokuwepo kwa utulivu.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya Dharura OCHA imesema mpango wa msaada unaohitaji takriban dola milioni 600 bado unaendelea.
Msemaji wa OCHA, Jens Laerke, akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi amesema “Kilichotokea kisiasa nchini Venezuela ni cha kushtua sana. Lakini kwa wananchi wengi, hali yao ya kila siku ya kibinadamu haijabadilika kwa kiasi kikubwa.”
Kati ya watu milioni nane wanaohitaji msaada, takriban 900,000 wana mahitaji makubwa sana katika sekta mbalimbali kama chakula, lishe, elimu na huduma za afya — mambo ambayo, kwa miaka kadhaa, serikali ya Venezuela imeshindwa kuwapatia raia wake.
Laerke aliongeza kuwa Venezuela ni miongoni mwa operesheni za misaada zinazopata ufadhili mdogo zaidi duniani, ingawa Umoja wa Mataifa umefanikiwa kuwafikia takriban watu milioni mbili kwa msaada hadi mwaka 2025.
Kusoma zaidi kuhusu Umoja wa Mataifa unavyoisaidia Venezuela bofya hapa taarifa ipo katika lugha ya kiingereza
Wakimbizi katika hali ya sintofahamu
Hali bado ni tete kwa mamilioni ya wakimbizi wa Venezuela wanaoishi nje ya nchi hiyo.
Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema kuwa hadi sasa hakuna wimbi kubwa la wakimbizi waliovuka mipaka kutokana na operesheni ya kijeshi ya Marekani.
Msemaji wa UNHCR, Eujin Byun, alisema shirika hilo linaendelea kufuatilia kwa karibu hali ilivyo mipakani na kushirikiana na mashirika mengine ya kibinadamu kusaidia na kulinda watu waliolazimika kuhama makazi yao.
Kwa mujibu wa UNHCR, takriban watu milioni 7.9 wameikimbia nchi yao ya Venezuela kutafuta hifadhi na maisha bora katika mataifa mengine, huku zaidi ya watu milioni 6.9 wakipata hifadhi katika nchi za Amerika ya Kusini na Karibiani.
UNHCR inaendelea kufanya kazi katika bara la Amerika na maeneo mengine kusaidia ujumuishaji wa raia wa Venezuela katika jamii zinazowapokea, pamoja na kutafuta suluhu za kudumu, kuimarisha utulivu na kuchochea maendeleo.