
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesikitishwa na tangazo la Ikulu ya Marekani juu ya uamuzi wa taifa hilo kujiondoa kutoka taasisi 66 za Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari jijini New York, hii leo kuwa tathmini ya michango ya nchi wanachama kwa bajeti ya Umoja wa Mataifa na ile ya ulinzi wa amani ni wajibu wa kisheria kwa wanachama wote ikiwemo Marekani kama ilivyoainishwa kwenye Chata ya Umoja wa Mataifa.
Kwa mantiki hiyo vyombo vyote vya Umoja wa Mataifa vitaendelea kutekeleza majukumu yao kama wanavyopatiwa na nchi wanachama.
Guterres amesema, “Umoja wa Mataifa una wajibu wa kutoa huduma kwa wale wanaotutegemea. Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa azma hiyo hiyo.”
Jana Jumatano Januari 7, Ikulu ya Marekani ilitoa orodha ya mashirika, vyombo na mikataba ya Umoja wa Mataifa kwa madai kwamba yanaenda kinyume na maslahi ya taifa hilo.
Mashirika hayo ni pamoja na lile la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA, Kituo cha Kimataifa cha Biashara, ITC, Kamati ya Maendeleo na Biashara, UNCTAD.
Vyombo vya Umoja wa Mataifa ni pamoja na Baraza la Uchumi na Kijamii, ECOSOC na Idara ya Uchumi na Kijamii, DESA.