Katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM Sofia ameeleza kuwa akiwa mtoto, aliona wanawake wakimsaidia mama yake kuzoea maisha mapya nchini Uingereza kuanzia kwenye kupanga miadi ya hospitali, kuandikisha watoto shule mpaka kujifunza jinsi ya kupata huduma za msingi. Msaada huo wa kijamii, ingawa ulikuwa wa kawaida, ulimfundisha thamani ya kuangalia mahitaji ya wengine na ulimjengea msingi wa maisha yake ya baadaye ya huduma kwa jamii.
Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, Safia alianza kusaidia familia mpya zilizokuwa zimewasili kwa kutafsiri miadi ya madaktari na mikutano mingine muhimu. Kupitia uzoefu huo, alijenga uelewa wa kina kuhusu ukosefu wa usawa uliokuwepo katika mifumo ya huduma, hali iliyompa hamasa ya kutaka kuboresha mifumo ambayo haikuwa ikihudumia kila mtu kwa haki.
Safia Jama, mzaliwa wa nchini Somalia na kiongozi wa diaspora anayeishi nchini Uingereza, ametumia zaidi ya miongo miwili kuwaunga mkono wanawake na familia kupitia juhudi zinazoongozwa na jamii.
Leo, Safia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kijamii la Women’s Inclusive Team (WIT), linalopatikana Tower Hamlets, mashariki mwa London. Alilianzisha mwaka 2003 kwa lengo la kusaidia wanawake kutoka asili mbalimbali katika moja ya maeneo yenye mchanganyiko mkubwa wa makabila kutoka kila kona ya dunia walioko nchini Uingereza. Mbali na hilo, Safia ni mwanaharakati, mpangaji wa shughuli za kijamii na mkufunzi wa afya ya akili.
Kwa kutambua mchango wake wa muda mrefu na athari chanya kwa jamii, Safia alitunukiwa tuzo ya “Member of the Most Excellent Order of the British Empire (MBE)” heshima ya kitaifa nchini Uingereza inayotolewa kwa watu waliochangia kwa kiwango cha juu katika jamii. Kazi yake pia imetambuliwa hadharani jijini London, ikiwemo na Shirika la Usafiri London (Transport for London), lililoliita jina lake treni nzima kama ishara ya kuthamini huduma yake wakati wa janga la coronavirus“>COVID-19.
Uwezo wa kuishi na kufanya kazi kati ya tamaduni mbili huwapa viongozi wa wahamiaji na diaspora mtazamo wa kipekee. Uzoefu wao wa maisha mara nyingi huwa kichocheo cha ubunifu, unaosaidia kuimarisha jamii, familia na huduma za kijamii, huku ukichangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.
“Nilipokuwa mama mwenye mtoto mchanga katika umri wa miaka ya ishirini, niligundua nguvu ya kujifunza kupitia michezo, hasa pale wanawake wanapopitia uzoefu huo pamoja,” Safia anakumbuka. Wakati huo, mbinu hizo hazikuwa zinapatikana kwa urahisi katika jamii zote, na akina mama wengi hawakuwa na maeneo salama ya kujifunza na kusaidiana.
Safia Jama, mzaliwa wa nchini Somalia na kiongozi wa diaspora anayeishi nchini Uingereza, ametumia zaidi ya miongo miwili kuwaunga mkono wanawake na familia kupitia juhudi zinazoongozwa na jamii.
Kwa kushirikiana na wanawake wengine, Safia alianza kuendesha vikao vidogo vilivyolenga malezi na kujifunza kwa njia ya michezo. Kilichoanza kama mikutano isiyo rasmi, baadaye kilikua na kuwa sehemu muhimu ya shughuli za Women’s Inclusive Team. Kadri shirika lilivyokua, programu hizo zilipanuka na kujumuisha fursa za ajira na ujuzi kwa wanawake katika jamii.
“Leo, kazi hii inatoa fursa zinazosaidia familia na pia kuboresha maisha ya kiuchumi,” Safia anasema.