Viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq wamesisitiza umuhimu wa kustawishwa na kuimarishwa ushirikiano wa pamoja baina ya nchi mbili kwa shabaha ya kudhamini uthabiti wa eneo.

Siku ya Jumapili, Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq aliwasili nchini Iran kwa lengo la kufautilia na kubadilishana mawazo na viongozi wa Iran kuhusu matukio ya eneo. Katika hatua ya kwanza ya kikazi ya safari yake ya siku mbili, alikutana na kuzungumza na Seyed Abbas Araghchi, Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.

Katika mikutano hiyo viongozi wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq wamesisitiza umuhimu wa kustawishwa na kuimarishwa ushirikiano wa pamoja.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa ameandamana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Araghchi amesema: Kukabidhiwa kambi ya Ain al-Asad iliyokuwa ikidhibitiwa na vikosi vya kijeshi vya Marekani kwa vikosi vya Iraq ni ishara nyingine ya kuimarishwa uhuru, uthabiti na kujitawala kisiasa Iraq.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa: Upeo na kina cha uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii kati ya Iran na Iraq ni wa aina tofauti, na kwamba mashauriano na mabadilishano ya mawazo kati ya viongozi wa nchi hizi mbili katika ngazi tofauti yanadhamini uimara na uratibu wa kutekelezwa uhusiano huo.

Spika wa Majlisi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia katika kikao chake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq kwamba: ‘Kulegeza msimamo kidogo tu dhidi ya utawala wa Kizayuni kutamaanisha kudhoofika kwa nchi zote za Kiislamu na hatimaye Umma wa Kiislamu.’

Qalibaf ameongeza kuwa: ‘Tunashuhudia walichokifanya Wazayuni kwa Syria na Iraq na hata kuishambulia Qatar kwa mabomu. Wamezigawanya Sudan na Somalia na hawana la kufanya zaidi ya kuudhoofisha na kuugawanya Umma wa Kiislamu kwa lengo la kuudhibiti.’

Fuad akiwa katika kikao na Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran mjini Tehran

Katika kikao hicho, Fuad Hussein sambamba na kuelezea furaha yake kuhusiana na safari yake nchini Iran na kuwasilisha ripoti kuhusu uchaguzi wa hivi karibuni wa Iraq amesema: ‘Usalama wa Iraq na Iran ni sehemu muhimu ya usalama wa eneo, na usalama wa nchi mbili hizi kimsingi unafungamana.’

Ziara ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq mjini Tehran na kutilia mkazo viongozi wa nchi mbili kustawishwa ushirikiano unaonyesha kuongezeka umuhimu wa uhusiano wa Iran na Iraq katika milingano ya kieneo. Kwa kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu changamoto na fursa, nchi hizi zinajaribu kuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuleta utulivu katika eneo kwa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi. Ushirikiano huu unaweza kuimarisha nafasi ya pamoja ya Tehran-Baghdad katika siku zijazo na kubuniwa mfumo wa kikanda wenye uwiano zaidi.

Zikiwa nchi mbili jirani zenye uhusiano wa kina wa kihistoria, kiutamaduni na kidini, Iran na Iraq ziko katika moja ya maeneo nyeti zaidi ya kijiopolitiki ulimwenguni. Matukio ya usalama katika Asia Magharibi, ushindani wa madola ya kikanda na nje ya kanda, na changamoto za pamoja za kiuchumi na kisiasa zimeweka udharura wa kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya Tehran na Baghdad.

Kupanuka ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa kati ya nchi hizi mbili si muhimu tu kwa utulivu wao wa ndani, bali pia kuna taathira za moja kwa moja kwa usalama na amani ya eneo zima.

Ushirikiano wa Tehran na Baghdad unaweza kupelekea kuundwa kwa mhimili thabiti na wenye ushawishi katika Asia Magharibi, mhimili ambao unaweza kukabiliana na changamoto za kiusalama, kiuchumi na kijiopolitiki za eneo na hivyo kuwa mkakati wa muda mrefu wa kuleta utulivu thabiti wa eneo.

Ushirikiano wa Tehran na Baghdad bila shaka utakuwa muhimu sana kwa nchi zote mbili na vile vile kwa eneo zima. Kuongezeka uthabiti wa kisiasa na kiusalama nchini Iraq, kupunguzwa ushawishi wa majeshi ya kigeni na kuimarishwa mhimili wa ushirikiano wa kieneo usiotegemea madola ya kigeni, yanahesabiwa kuwa matokeo muhimu zaidi ya kuimarishwa uhusiano wa Iran na Iraq katika nyuga za kisiasa, kiusalama na kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *