Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani uamuzi wa hivi karibuni wa Argentina wa kuituhumu sehemu ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), na kuutaja uamuzi huo kuwa usioweza kuhalalishwa, na ni hatari kwa usalama wa taifa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya ya Iran imetoa taarifa ikilaani hatua za Argentina na kuzitaja kuwa kinyume cha sheria na zinazotekelezwa kutokana na mashinikizo kutoka nje, hususan kutoka kwa utawala wa Kizayuni, baada ya serikali ya Argentina, siku ya Jumamosi, kukitaja Kikosi cha Quds cha jeshi la IRGC na shakhsia 13 kuwa magaidi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kuwa uamuzi huo sio tu unahatarisha uhusiano wa nchi mbili lakini pia unaacha mfano tata katika diplomasia ya kimataifa ambayo matokeo yake ya kisheria na kisiasa yatabaki kwa serikali ya Argentina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekosoa madai kuhusu shambulio la bomu la mwaka 1994 katika Kituo cha Kiyahudi cha Argentina (AMIA), ikihusisha kushindwa kupatiwa ufumbuzi kesi hiyo kuwa kunatokana na msukumo wa kisiasa na rushwa ndani ya mfumo wa mahakama wa Argentina.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema hatua zote hizi zinalenga kupotosha ukweli na kuwaficha wahusika halisi wa tukio hilo.

Mwezi Julai mwaka 1994 Kituo cha Wayahudi cha Argentine Israelite Mutual Association (AMIA) huko Buenos Aires kililengwa na shambulio la bomu, ambapo watu 85 waliripotiwa kuuawa na wengine 300 kujeruhiwa.

Hakuna upande uliodai kuhusika na shambulio hilo la bomu ingawa Israel imekuwa ikiituhumu Iran katika uwanja huo. Tehran imekanusha mara kadhaa madai hayo katika miongo mitatu iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *