
Bayern itaungana na Arsenal kufuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo, Januari 21, 2025 ikiwa itaibuka na ushindi nyumbani dhidi ya Royale Union SG lakini hilo litatimia kama Liverpool na Atletico Madrid zitashindwa kupata ushindi kwenye mechi zao.
Ushindi wa nyumbani leo dhidi ya Royale Union SG ya Ubelgiji, utaifanya Bayern kufikisha pointi 18 na hivyo kujihakikishia kumaliza katika nafasi nane za juu kwenye msimamo wa Ligi ya Mashindano hayo lakini ni iwapo tu Atletico Madrid na Liverpool ama zitafungwa au kutoka sare leo.
Lakini iwapo Liverpool na Atletico Madrid zitapata ushindi, Bayern italazimika kusubiri hadi raundi ya mwisho ambapo itatakiwa kupata sare au ushindi iweze kusonga mbele.
Liverpool ambayo imekusanya pointi 12 katika mashindano hayo, leo itakuwa ugenini huko Ufaransa kukabiliana na Olympique Marseille.
Atletico Madrid nayo itakuwa na kibarua ugenini huko Uturuki ambako itaumana na Galatasaray ikihitaji ushindi ambao utaweka hai matumaini yake ya kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora na sio kwa kutegemea mechi za mchujo.
Mechi nyingine ya kuvutia leo ni baina ya Juventus na Benfica ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Allianz jijini Turin.
Wakati Juventus ikisaka ushindi ambao utaifanya angalau ibaki na matumaini ya kucheza hatua ya mchujo, Benfica nayo itakuwa na ndoto kama hizo ingawa ikitoka sare au kupoteza itakuwa imeaga rasmi mashindano hayo.
Jana Arsenal ilikuwa timu ya kwanza kujihakikishia kuingia hatua ya 16 bora baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 ugenini mbele ya Inter Milan.
Wakati Arsenal ikitinga hatua inayofuata, timu za Kairat Almaty na Villarreal zimeaga rasmi mashindano hayo msimu huu.
RATIBA YA MECHI ZA LEO LIGI YA MABINGWA ULAYA
Galatasaray vs Atletico Madrid (Saa2:45 usiku)
Qarabag vs Eintracht Frankfurt (Saa 2:45 usiku)
Atalanta vs Athletic Bilbao (Saa 5:00 usiku)
Bayern vs Royale Union SG (Saa 5:00 usiku)
Chelsea vs Pafos (Saa 5:00 usiku)
Juventus vs Benfica (Saa 5:00 usiku)
Marseille vs Liverpool (Saa 5:00 usiku)
Newcastle United vs PSV (Saa 5:00 usiku)
Slavia Prague vs Barcelona (Saa 5:00 usiku)