“Bodi ya Amani imeundwa kwa mujibu wa mpango uliowasilishwa kwa Baraza la Usalama, kupigiwa kura na kukubaliwa,” amesema Srinivasan Muralidhar, Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi kuhusu Ardhi ya Palestina Inayokaliwa na Israel, ikiwemo Jerusalem Mashariki.
“Kwa upande wetu kama Tume ya Uchunguzi, tunaona jukumu letu ni kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu. Na hilo ndilo jukumu tulilopewa na Umoja wa Mataifa” ameongeza
Tume ya Uchunguzi moja ya mifumo ya juu ya uchunguzi ya Baraza la Haki za Binadamu iliundwa na Nchi Wanachama 47 wa baraza hilo Mei 2021.
Mwezi Novemba mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio namba 2803, likikaribisha kuanzishwa kwa Bodi ya Amani kama “utawala wa mpito wa kusimamia ujenzi mpya wa Gaza.”
Dai la mauaji ya kimbari
Septemba mwaka jana, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, na aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay, alitangaza kuwa Israel ilitekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas ambayo yalisababisha vifo vya takribani watu 1,200 nchini Israel Oktoba 2023 na kuchochea vita. Israel ilikanusha vikali dai hilo.
“Tunahitaji kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na wahusika wote wenye wajibu na katika maeneo yote mawili,” amesema Bwana Muralidhar, akieleza matumaini kuwa matokeo ya awali ya Tume “yataingia katika mifumo ya kisheria ya kutoa haki ya kudumu kwa watu wa maeneo haya mawili.”
Katika ajenda ya mwaka huu, Tume inapanga pia kuchunguza “mashambulizi ya wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya watu wengine ndani ya maeneo haya mawili,” amesema, akisisitiza uhuru wa jopo hilo.
Akijibu maswali kuhusu Bodi ya Amani, mchunguzi mkuu amesema anatarajia mpango wa amani unaotekelezwa “uzingatie maslahi ya watu wote walioko katika eneo la mgogoro.”
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, jopo la wataalamu huru wa haki za binadamu ambao hawafanyi kazi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na hawalipwi pia wamelaani mauaji yaliyoripotiwa ya waandishi wa habari watatu wa Kipalestina katika eneo la Gaza ya kati, waliouawa katika shambulio la anga la Israel jana Jumatano.
“Unapomuua mwandishi wa habari, inamaanisha una kitu cha kuficha,” amesema Kamishna Florence Mumba.
Watoto katika Gaza huhudhuria madarasa katika nafasi ya kujifunza ya muda iliyofunguliwa na Umoja wa Mataifa.
Mtazamo kwa UNRWA
Jopo hilo pia limetoa maoni yake kuhusu uharibifu mkubwa wa makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, katika eneo la Jerusalem Mashariki inalolikalia, jana Jumatano, likisisitiza nafasi yake muhimu ya kusaidia Wapalestina kwa miongo kadhaa.
“Israel inapaswa kufikiri kwa makini kabla ya kukataa kazi ambayo UNRWA imefanya, kazi muhimu ambayo imeipunguzia Israel baadhi ya wajibu wake,” amesema Chris Sidoti. “Bila shaka, kutakuwa na athari mbaya kwa haki za binadamu watoto wana haki ya elimu, na watu wote wana haki ya kufikia kiwango cha juu kinachowezekana cha afya ya mwili na akili.”
Bi. Pillay alistaafu Oktoba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 83, akifuatiwa na makamishna wenzake Chris Sidoti na Miloon Kothari.
Mwezi Novemba mwaka jana, jopo jipya liliteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu likimrejesha Bwana. Sidoti pamoja na majaji wenzake Bwana. Muralidhar kutoka India na Bi. Mumba kutoka Zambia.
Mwenyekiti wa Tume alibainisha kuwa upungufu wa ufadhili umezuia jopo hilo kuchunguza usambazaji wa silaha na vurugu za walowezi, licha ya kuwa sehemu ya jukumu walilopewa na Baraza la Haki za Binadamu.
“Kwa sababu ya ukosefu wa fedha, hatukuweza kuingia katika maeneo hayo,” ameeleza Bwana. Muralidhar kwa waandishi wa habari.