KWA kawaida mchezo wa kikapu umezoeleka ili kuucheza ni lazima uwe na mwili mkubwa, hususan urefu.

Lakini, hiyo haizuii mchezaji mfupi kuucheza vyema ilimradi awe na uwezo na ubora unaotakiwa kufanikisha matokeo na ufanisi wa timu.

Mchezaji mfupi wa kikapu anayecheza nafasi ya namba moja maarufu zaidi kama point guard hupata wakati mgumu kucheza nafasi nyingine kutokana na umbile lake na hata udogo wa mwili. Ugumu wa kucheza nafasi nyingine, kama ilivyo namba nne maarufu kama power forward, unatokana na umbile la ukubwa wa mwili unaohitajika.

Katika nafasi hiyo, mchezaji mrefu ndiye anayetakiwa kucheza. Sifa yake ni kuwa na uwezo wa kucheza nafasi ya chini (post player), na kama jina lake linavyoeleza, anatakiwa pia awe na nguvu zaidi ya kupambana kufunga karibu na kikapu pamoja na kukamata mipira inayodunda (rebound).

Baadhi ya wachezaji wa Tanzania ambao ni wafupi na wanaocheza nafasi ya namba 1, yaani Point Guard, ni Ally Faraji kutoka timu ya Dar City, Josephat Peter (UDSM), Sponcian Ngoma (Srelio) na Omary Ndulla (JKT).

KIKA 01

Kwa wanaofuatilia Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA), bila shaka mifano ya wachezaji hao itawafanya kuelewa kwa nini wanaitwa point guard kwenye timu wanazochezea. Baadhi yao ni Stephen Curry wa Golden State Warriors, Trae Young aliyekuwa Atlanta Hawks kabla ya kuhama hivi majuzi, Luka Doncic wa Los Angeles Lakers, Devin Booker wa Phoenix Suns, Kyrie Irving wa Dallas Mavericks na wengineo wengi.

Akizungumzia hilo, kocha mkongwe wa mpira wa kikapu nchini, Bahati Mgunda anasema japo mchezaji yeyote anaweza kucheza nafasi zote uwanjani, lakini kwenye nafasi ya chini kunakuwa na ugumu.

“Kama ni mchezaji mfupi inakuwa ngumu kucheza nafasi ya chini, kama walivyo baadhi ya wachezaji wetu ambao ni wafupi. Japo ukishakuwa mchezaji wa kikapu unaweza kucheza nafasi yoyote,” anasema Bahati.

Kwa mujibu wa Mgunda kitakachomfanya mchezaji acheze nafasi zote ni uwezo wa kimchezo pamoja na umbo alilonalo sambamba na jinsi ya kucheza kulingana na ubora akitoa mfano wa Tyrone Edward anayechezea Stein Warriors kuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza nafasi zote za uwanjani kutokana na umbile lake.

KIKA 02

Kocha Salum Issa anasema mchezaji mwenye uwezo wa kucheza namba nne (power forward) anatakiwa awe na urefu zaidi ya futi sita. “Kwa ujumla mchezaji anayecheza kama namba nne (power forward), ni vyema zaidi awe mrefu, mwenye mwili (mkubwa) na hata nguvu zaidi ili iwe rahisi kwake kudaka na kunyang’anya mipira kama zile rebound,” anasema Salumu.

Kocha huyo anasisitiza kuwa mchezaji husika lazima awe na sifa hizo ili kucheza katika nafasi ya chini, kwa lengo la kufunga karibu na kikapu, mbali na uwezo wa kucheza mipira ya kushambulia (offensive rebound).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *