“Mwaka 2026 tayari unaonekana kuwa mwaka wa machafuko na mshangao wa mara kwa mara,” amewaambia waandishi wa habari jijini New York.
Bwana Guterres aliyesomea fizikia kabla ya kuingia kwenye maisha ya umma amesema kuwa katika nyakati za mabadiliko makubwa, hurejea kwenye kanuni thabiti zinazoeleza jinsi nguvu zinavyofanya kazi.
Kuchagiza hatua chanya
Miongoni mwa kanuni hizo ni Sheria ya Tatu ya Mwendo ya Newton, inayosema kwamba kwa kila tendo kuna majibu sawa na ya kinyume.
Amesema “Tunapoanza mwaka huu, tumeazimia kuchagua hatua zitakazochagiza hatua halisi na chanya”.
Katibu Mkuu amezitaja hatua hizo kuwa ni “Hatua za amani, za haki, za uwajibikaji, na za maendeleo katika nyakati zetu zenye misukosuko.”
Mwanamke mmoja mzee anakunywa kinywaji chenye joto katika kambi ya wakimbizi nchini Ukraine.
Mnyororo wa athari
Leo, kutokuwajibika kunachochea migogoro amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa kikichangia kuongezeka kwa mapigano, kupanua wigo wa kutoaminiana, na kuruhusu waharibifu wenye nguvu kuingilia kutoka pande zote.
“Wakati huohuo, kupunguzwa kwa msaada wa kibinadamu kunazalisha mnyororo wake wa athari mbaya za kukata tamaa, ufurushwaji wa watu, na vifo, huku ukosefu wa usawa ukiendelea kuongezeka”.
Guterres pia ameangazia mabadiliko ya tabianchi “mfano halisi na wenye uharibifu zaidi wa kanuni ya Newton” akisema kuwa hatua zinazopasha joto sayari zinasababisha dhoruba, moto wa nyika, vimbunga, ukame na kupanda kwa kina cha bahari.
Mabadiliko ya kipekee
Dunia pia inashuhudia “pengine uhamisho mkubwa zaidi wa nguvu katika nyakati zetu”, amesemayaani kutoka kwa serikali kwenda kwa makampuni binafsi ya teknolojia.
Ameonya kuwa “Wakati teknolojia zinazounda mienendo ya tabia, chaguzi, masoko, na hata migogoro zinafanya kazi bila vizingiti, hatua zake si ubunifu, bali ni kuyumba.”
Lazima kubadilika Kwenda na wakati
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu changamoto hizi zinatokea wakati mifumo ya kutatua matatizo ya kimataifa bado inaakisi miundo ya kiuchumi na nguvu ya miaka 80 iliyopita na hali hiyo lazima ibadilike.
“Mifumo na taasisi zetu lazima ziakisi ugumu na fursa za nyakati na uhalisia huu mpya,” amesema akiongeza kuwa “Matatizo ya kimataifa hayatatatuliwa na nguvu moja kuamua kila kitu. Wala hayatatatuliwa na nguvu mbili kugawanya dunia katika maeneo hasimu ya ushawishi.”
Amesisitiza umuhimu wa kuharakisha ulimwengu wa kimataifa “ulio na mtandao, unaojumuisha wote kwa muundo, na wenye uwezo wa kuleta uwiano kupitia ushirikiano” lakini akabainisha kuwa peke yake hauhakikishi uthabiti wala amani.
“Ili ushirikiano wa kimataifa ulete uwiano, ustawi na amani, tunahitaji taasisi imara za kimataifa zenye uhalali unaotokana na uwajibikaji wa pamoja na maadili ya pamoja,” amesema.
Maadili ya pamoja
Aidha, katika juhudi za mageuzi, “miundo inaweza kuwa imepitwa na wakati lakini maadili hayajapitwa na wakati,” amesema Katibu Mkuu.
Jeshi la MINUSCA linachunguza mpaka wazi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan.
Kwa muktadha huo, alisema kuwa waliounda Mkataba wa Umoja wa Mataifa “walielewa kuwa maadili yaliyoainishwa katika nyaraka zetu za msingi hayakuwa dhana za juu au matumaini ya kiitikadi, bali lilikuwa sharti lisiloweza kuepukika kwa amani ya kudumu na haki endelevu.”
Amesema “licha ya vikwazo vyote, Umoja wa Mataifa unaendelea kuchukua hatua kuhuisha maadili yetu ya pamoja na hautakata tamaa”.
Amani, mageuzi na maendeleo
“Tunasisitiza amani ya haki na endelevu inayojengwa juu ya sheria za kimataifa. Amani inayoshughulikia chanzo cha migogoro. Amani inayodumu zaidi ya kutiwa saini kwa makubaliano.”
Umoja wa Mataifa pia unaendelea kusukuma mageuzi na uimarishaji wa Baraza la Usalama “chombo pekee chenye mamlaka ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kuhusu amani na usalama kwa niaba ya kila nchi.”
Akisema kuwa hakuna amani ya kudumu bila maendeleo, ameangazia juhudi za kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na mageuzi ya mfumo wa kifedha wa kimataifa.
“Hii inajumuisha kukomesha mzunguko mzito wa madeni, kuongeza mara tatu uwezo wa utoaji mikopo wa benki za maendeleo za kimataifa, na kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata ushiriki wa haki na ushawishi wa kweli katika taasisi za kifedha za kimataifa,” amesema.
Mnamo Januari 17, 2026, barabara zinafurika baada ya mvua kubwa huko Buzi, Mkoa wa Sofala, Msumbiji.
Msaada kwa tabianchi
Kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, amesisitiza haja ya kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa hewa chafuzi katika muongo huu, pamoja na mpito wa haki na usawa kutoka nishati ya mafuta kisukuku kwenda nishati mbadala.
“Tunahitaji msaada mkubwa zaidi kwa nchi ambazo tayari zinakabiliwa na janga la tabianchi, kupanua wigo wa mifumo ya tahadhari za mapema, na kutoa fursa kwa mataifa yenye rasilimali muhimu za madini kupanda katika minyororo ya thamani ya kimataifa,” amesema.
Umoja wa Mataifa pia unafanya kazi kwa dharura kuelekea mfumo wa usimamizi wa teknolojia, ikiwemo kupitia mazungumzo ya kimataifa, msaada wa kujenga uwezo, na Jopo jipya la Kimataifa la Kisayansi kuhusu Akili Mneba AI.
Majina ya wajumbe 40 waliopendekezwa kwa ajili ya jopo hilo yatawasilishwa hivi karibuni kwa Baraza Kuu.
AI kwa ulimwengu unaoendelea
Bwana. Guterres pia ametoa wito wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa Kujenga Uwezo wa AI kwa nchi zinazoendelea, ukiwa na lengo la dola bilioni 3.
Amesema “Tunapoanza mwaka huu, tumeazimia kuchagua hatua zitakazozalisha hatua halisi na chanya”.
Ametaja hatua hizo kuwa ni “Hatua za amani, za haki, za uwajibikaji, na za maendeleo katika nyakati zetu zenye misukosuko.”