Kwa mujibu wa OCHA watu hao wamekimbia kufuatia mapigano ya hivi karibuni katika majimbo ya Aleppo, Hasakeh na Raqqa, katikati ya msimu wa baridi kali.

Mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa hali bado haijatengamaa, huku watu waliokimbia makazi yao wakikabiliwa na msongamano mkubwa kwenye makazi ya muda na mahitaji ya kibinadamu yakiongezeka kwa kasi kila uchao.

Hatua za dharura

OCHA na washirika wengine wa kibinadamu wanaendelea kuimarisha hatua zao za dharura huku wakikabiliana na athari za dhoruba kali za msimu wa baridi vilivyokumba maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Hali mbaya ya hewa imezidisha changamoto za kufikia maeneo yaliyoathirika, kuharibu miundombinu, na kuongeza hatari kwa jamii zilizoathiriwa na mzozo limesisitiza shirika hilo.

Wiki hii, msafara wa misaada wa mashirika mbalimbali uliondoka katika mji mkuu wa Syria Damascus na kuwasili Qamishli, katika jimbo la Hasakeh.

Mizigo ya msaada huo ilijumuisha chakula, mavazi ya kujikinga na baridi, mablanketi na mahitaji mengine ya msingi.

Misafara mingine imepangwa kufanyika siku zijazo, huku usambazaji wa chakula, mikate na msaada wa kifedha ukiendelea katika vituo na maeneo yanayohifadhi wakimbizi wa ndani.

Huduma za afya na nyingine viko katika shinikizo

Kwa mujibu wa jumuiya ya kibinadamu, hali bado ni tete katika majimbo kadhaa, hususan Hasakeh, ambako vituo vingi vya mapokezi bado vimejaa kupita pomoni.

Washirika wa Umoja wa Mataifa waliopo eneo hilo wanatoa huduma za afya kwa njia ya kliniki tembezi, ikiwemo chanjo na huduma za afya ya akili.

Sekta ya lishe pia imeimarishwa, na kuwafikia zaidi ya watoto 1,500 pamoja na mamia ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika jimbo la Hasakeh.

Kwa mujibu wa OCHA, huduma pia zinaathiriwa na dhoruba kali ya msimu wa baridi iliyokumba majimbo kadhaa ya Syria wiki iliyopita.

Njia kuu za milimani bado zimefungwa, na hivyo kuzitenga jamii katika miji ya Latakia na Tartus.

Katika mijii ya Hama na Homs, mafuriko na barabara zilizozibwa zinaendelea kuzuia ufikiaji wa maeneo yaliyoathirika.

Tangu Oktoba mwaka jana, washirika wa kibinadamu wametoa msaada wa msimu wa baridi ikiwemo mablanketi, mavazi ya kujikinga na baridi, na vifaa vya kupasha joto kwa takriban watu 450,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *