
Kocha wa Senegal, Pape Thiaw, amewaomba mashabiki kusitisha kampeni ya kuchangisha fedha ili kulipia faini ya Dola 100,000 (Sh256 milioni) aliyotozwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kufuatia matukio yaliyojitokeza katika Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Katika fainali hizo zilizofanyika Morocco, Thiaw aliiongoza Senegal kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco, na hivyo kuipatia nchi hiyo taji la mashindano hayo.
Juzi Jumatano, Januari 28, 2026, CAF ilimpa Thiaw adhabu kali ya kumsimamisha mechi tano katika mashindano rasmi ya shirikisho hilo na pia kumtoza faini ya kiasi hicho cha fedha.
Baada ya adhabu hiyo, mashabiki wa Senegal walianzisha kampeni ya mtandaoni kumsaidia kocha huyo kulipa faini, wakionyesha kuvutiwa na mshikamano wao kwake.
Hata hivyo, Thiaw aliwahi haraka kutambua ishara hiyo huku akiomba kwa unyenyekevu wafuasi waelekeze rasilimali zao kwenye sababu zilizo na uhitaji mkubwa zaidi.
Akiandika kwenye akaunti yake binafsi ya Instagram, Thiaw amesema kuwa anashukuru kwa thamani ambayo mashabiki wa Senegal wanamuonyesha lakini anaomba wasichangishe fedha kwa ajili yake na badala yake wafanye hivyo kwa watu wenye uhitaji maalum.
“Watu wa Senegal, familia yangu, mshikamano wenu tangu kutangazwa kwa adhabu hizi unagusa sana moyo wangu. Asanteni kwa upendo mnaonionyesha kila siku.
“Hata hivyo, nawaomba kwa unyenyekevu msiandae kampeni za kuchangisha fedha kwa jina langu. Ingawa ninaelewa na kuthamini ukarimu huu mkubwa, nawahimiza kuelekeza fedha hizi kwenye sababu za dharura zaidi, mkisaidia wale walio katika uhitaji mkubwa zaidi,” amesema Thiaw.
Adhabu ya kusimamishwa mechi tano inahusu mashindano ya CAF pekee, ikimaanisha kuwa Thiaw ataendelea kuwa na sifa za kuiongoza Senegal katika Kombe la Dunia 2026 majira ya joto yajayo.
Mbali na adhabu hiyo ya Thiaw, Shirikisho la Mpira wa Miguu Senegal (FSF) lenyewe limepewa adhabu ya faini kiasi cha Dola 615,000 (Sh1.6 bilioni) kwa makosa matatu ambayo ni vurugu za mashabiki wa timu ya taifa ya nchi hiyo, vitendo vya utovu wa nidhamu vya wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la timu yao kwenye fainali hiyo pamoja na wachezaji wake watano kuonyeshwa kadi za njano.
Pia wachezaji wa Senegal, Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr kila mmoja amefungiwa michezo miwili rasmi ya CAF kwa utovu wa nidhamu wa kumshambulia Refa wa mchezo.