Iwe wewe ni “mwenye hofu au mwenye matumaini” kuhusu mada hii, haiwezekani kupuuza AI, ambayo inaingia katika kila pembe ya maisha yetu binafsi na ya kikazi.
Kwa muda sasa, Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza umuhimu wa mtazamo wa “binadamu kwanza kuhusu AI”. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alionya Baraza la Usalama mwaka 2024 kwamba hatima ya ubinadamu “haitakiwi kamwe kuachwa mikononi mwa sanduku jeusi la algoriti,” na kwamba wanadamu lazima wabaki na usimamizi na udhibiti wa maamuzi ya AI ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa.
Akili Mnemba sasa inabadilisha sekta ya simu ya rununu.
Tangu wakati huo, mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kazi ya kuendeleza aina ya utawala wa kimataifa wa kimaadili wa Akili Mnemba, kwa kujenga juu ya miongozo na mapendekezo yaliyomo katika Mkataba wa Kidijitali wa Kimataifa (Global Digital Compact).
Haya hapa ni baadhi ya mawazo muhimu.
1. Elimu ni ufunguo
Umoja wa Mataifa mara kwa mara husisitiza kuwa elimu ni nguzo kuu ya kuhakikisha watu wanabaki na umuhimu katika mustakabali unaowezeshwa na AI. Hili si suala la kuingiza tu zana za AI katika mifumo ya elimu, bali ni kuhakikisha wanafunzi na waelimishaji wanakuwa na uelewa na ujuzi wa AI.
“Mfumo wa elimu duniani utahitaji walimu milioni 44 ifikapo mwaka 2030,” anasema Shafika Isaacs, mkuu wa teknolojia na AI katika elimu huko UNESCO shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni.
Ameongeza kuwa “Tunaamini ni kosa kusema kwamba tunapaswa kuwekeza zaidi katika teknolojia za AI badala ya kuwekeza kwa walimu. AI inaweza kusimamia uhamishaji wa data, lakini haiwezi kusimamia maendeleo ya binadamu. Elimu kimsingi ni uzoefu wa kijamii, kibinadamu na kitamaduni, si upakuaji wa kiufundi.”
2. Kukubali mabadiliko
Watu wengi duniani wana wasiwasi wa kupoteza ajira zao kutokana na teknolojia hii. Hili halishangazi, ikizingatiwa kuwa Jukwaa la Uchumi Duniani WEF, lilikadiria mwaka 2025 kwamba takribani asilimia 41 ya waajiri walipanga kupunguza wafanyakazi wao kutokana na AI.
Wakati huohuo, majukumu mapya yanayolingana na nguvu za binadamu pamoja na uwezo wa mashine yanatarajiwa kuibuka. Ingawa mashine ni bora katika kutambua mifumo na kufanya kazi za kurudia-rudia, hazina uwezo mkubwa katika ubunifu, maamuzi ya busara, hoja za kimaadili, na mwingiliano tata wa kibinadamu.
GPU hutumiwa kufunza miundo ya AI kwa kufanya shughuli changamano za hisabati.
Kwa kushirikiana na washirika wa utafiti wa kimataifa, Shirika la Kazi la U moja wa Mataifa Duniani ILO, limetabiri kwamba ingawa takribani kazi moja kati ya nne itabadilishwa na AI, hili halimaanishi lazima kuwepo kwa upotevu wa jumla wa ajira.
Hata hivyo, namna kazi inavyofanywa ina uwezekano wa kubadilika kwa kiasi kikubwa, na hivyo kuwaweka wafanyakazi katika jukumu la kuwa wepesi wa kuzoea mabadiliko, na kuwa tayari kujifunza ujuzi mpya na kupata mafunzo endelevu katika maisha yao ya kazi.
3. Kuhakikisha AI inapatikana kwa wote
Makampuni machache makubwa ya teknolojia yanaongoza utafiti wa AI na kutawala uundaji wa zana mpya. Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba, endapo upatikanaji wa teknolojia hii hautapanuliwa, pengo la usawa kati ya nchi na ndani ya jamii litaongezeka.
Mikakati iliyotengenezwa na Umoja wa Mataifa inasisitiza kuwa sera za elimu, uchumi na utawala zinapaswa kuhakikisha manufaa ya AI yanawanufaisha watu wengi, na si kubaki kwa waliobahatika au wale walioko mbele kiteknolojia pekee.
4. Kuweka haki za binadamu mbele
Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza mara kwa mara kwamba maendeleo ya AI lazima yaheshimu haki za binadamu, utu na ujumuishwaji, na imeonya kuwa mifumo ya kiautomatiki isiyodhibitiwa inaweza kuongeza migawanyiko ya kijamii.
Mifumo ya AI itasaidia katika uchambuzi wa takwimu, kufanya maamuzi, automatisering, na optimization.
Mwaka 2021, baada ya mashauriano ya kina na wataalamu wa kimataifa, UNESCO ilitoa pendekezo kuhusu Maadili ya Akili Mnemba, likisisitiza kuwa haki za binadamu haziwezi kuwa chaguo la kimaadili tu, bali lazima ziwe msingi wa lazima wa mifumo ya AI.
Hati hiyo shirika hilo linasema kuwa zana zinazotishia utu, usawa au uhuru zinapaswa kudhibitiwa au kupigwa marufuku, na kwamba serikali lazima zisimamie kikamilifu utekelezaji wa viwango hivi.
5. Dunia inahitaji kukubaliana mwelekeo wa pamoja
Hili si suala ambalo serikali ya kitaifa, sekta binafsi au asasi za kiraia zinaweza kulikabili peke yao, na Umoja wa Mataifa unatoa wito wa ushirikiano wa kimataifa.
Hii inaweza kujumuisha majadiliano kuhusu utawala na maadili, majukwaa yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya uratibu, pamoja na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kufadhili elimu na maendeleo ya nguvu kazi.
Katika kituo cha takwimu, seva ni kompyuta zenye utendaji wa juu zinazochakata na kuhifadhi takwimu muhimu.
Je, Afrika inaweza kukwepa pengo linaloongezeka?
Kwa Afrika, ambako miundombinu ya kidijitali, upatikanaji wa data na mapengo ya ujuzi bado hayalingani, zama za akili mnemba ni wakati wa matumaini makubwa lakini pia wa hatari.
Utawala wa data, upendeleo wa algoriti, kuhamishwa kwa ajira na uwezo mdogo wa udhibiti ni miongoni mwa changamoto kuu zinazowakabili watunga sera barani Afrika.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Afrika ina takribani asilimia 18 ya idadi ya watu duniani, lakini inawakilisha chini ya asilimia moja ya uwezo wa vituo vya data duniani. Hii inaashiria kuwa bara linaweza kuwa zaidi mtumiaji wa teknolojia za AI zilizotengenezwa kwingineko, badala ya kuwa mtengenezaji anayezibuni kulingana na mahitaji ya ndani.
Kwa upande chanya, AI inaweza kuwa muhimu katika kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Afrika kwa manufaa ya wote. Kuna mifano mingi chanya ya matumizi ya AI kuboresha maisha, kuanzia mifumo ya tahadhari ya mapema inayosaidia kutabiri ukame katika Pembe ya Afrika, hadi zana za kujifunza kwa mashine zinazoboresha ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa.
Ufunguo wa kuhakikisha Afrika inanufaika na fursa hizi ni kuwekeza katika data za ndani, ujuzi na utafiti, pamoja na mifumo ya AI iliyo jumuishi na ya lugha nyingi. Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA) imeeleza kuwa matumizi ya AI katika kilimo, afya, ufuatiliaji wa hali ya hewa na huduma za umma yanaweza kusaidia nchi “kuruka njia za jadi za maendeleo na kukumbatia uwezo wa AI.”