Chui mamas wawavutia watalii, wadumisha utamaduni wa kimasaiChui mamas wawavutia watalii, wadumisha utamaduni wa kimasai

Wanawake hao wa Kimasai wanaofahamika zaidi kama “Chui Mamas” wanajenga manyatta za kitamaduni na kuwapokea wageni kwenye sehemu maalum iliyotengwa kama kijiji cha watalii. Chui Mamas wanaotumia mila na sanaa kuhifadhi tamaduni zao. 

Kijijini Koija, katika kaunti ya Laikipia utajiri mkubwa wa mila na tamaduni umeleta tija kwa kikundi kimoja cha kujitegemea. Jamii za wamasai zilizoko hapa zinaishi kama ilivyokuwa zamani na kufuata utaratibu wa kiasili. Chui Mamas wanasimamia na kuendesha kijiji maalum cha kiasili ambako huwapokea wageni na watalii wanaotaka kuelewa utamaduni wa kimaasai.

Senketo ni muweka hazina wa Chui Mamas na anaeleza kuwa wageni wanapata fursa ya kuelewa utamaduni wao kwa kuwatembelea:

” Tuna kundi la warani , wanaimba na kuwatumbuiza wageni kisha wanalipwa. Wao kama kina mama wanavaa sare zao za kitamaduni jambo linalowavutia wageni wanaowaachia hela. Hio ndio shughuli yao ya kwanza,” alisema Senketo.

Umuhimu wa shanga katika utamaduni wa Kimasai

Kenya | wanawake wa Kikundi cha Chui Mamas wanaotangaza utamaduni wao
Kikundi cha Chui Mamas wanaonadi utamaduni na mila za kimasai kama kitega uchumi huko Koija, Laikipia nchini Kenya.Picha: Thelma Mwadzaya/DW

Shanga zina umuhimu mkubwa katika utamaduni wa kimaasai. Chui Mamas hutunga shanga za kila rangi mahsusi kuvaa shingoni, kichwani, miguuni maarufu kama vikuku, mikanda na bangili. Bidhaa hizo za nakshi huwa na rangi za kuvutia na kila moja ina maana muhimu katika jamii ya  waMaasai. 

Shanga nyeupe zinaashiria usafi na afya, nyekundu ni ujasiri na nguvu, samawati huwakilisha nguvu na mbingu, kijani ni lishe na ardhi, manjano ni ya ukarimu na usuhuba,  rangi ya machungwa ni uzazi na jua,  na nyeusi ni umoja na maelewano katika jamii.

Wamaasai huvaa shanga za rangi zote hizo kuwasilisha ujumbe kuwa ni wakarimu na watu walio na roho safi. Chui Mamas walianza kwa kuchangisha hela ili kununua shanga na ndipo mradi wa kiasili ukaibuka. Wangoi Naputari ni mmoja ya viongozi wa Chui Mama na anasimulia umuhimu wa kukifunza kizazi kijacho utamaduni huu muhimu.

Wangoi anasema wanaendelea kuwafunza watoto wao jinsi ya kutunga shanga za kitamaduni ila hawangependa watoto hao wathamini pesa wakiwa na umri mdogo. Huagizwa kutunga shanga na hukumbushwa kuwa sio zake.

” Watoto huambiwa kuwa wanamsaidia mama kutengeza shanga kisha mapato yake yanatumika kulipia karo ya shule na chakula. Muhimu wanatakiwa kutia juhudi kwenye masomo ila tunawafunza utamaduni huu, ” alisema mwanamke huyo.

Kujipatia kipato kupitia bidhaa za kiasili

Kenya. Laikipia 2026 | Manyatta iliyoko kwenye Kijiji cha kitamaduni cha Chui Mamas
Manyatta iliyoko kwenye Kijiji cha kitamaduni kinachosimamiwa na Chui Mamas huko Koija, Laikipia.Picha: Thelma Mwadzaya/DW

Bidhaa za kiasili huwapa wanawake wa Chui Mamas sauti katika jamii kwa kuwaongezea kipato na pia kudumisha utamaduni wa kimaasai. Matokeo ya juhudi zote hizi ni kuwa sasa wana sauti katika jamii na uhusiano kati ya wanawake na wanaume umeimarika kwa kiasi kikubwa kama anavyosimulia Senketo wa kikundi cha kujitegemea cha Chui Mamas anasema kwa sasa wazee hawana tatizo. Wanaweza kusafiri hadi ng’ambo na waume zao hawana wasiwasi wowote.

“Tunasafiri wakati wowote. Unajua katika mila za waMaasai, wanaamini kuwa mwanamke akiondoka basi anaenda kutangatanga. Siku hizi wamebadilika na wanaipenda hii kazi kwani wameiona faida yake, ” aliongeza Senketo.

Mbali ya kunadi utamaduni wa kiMaasai, Chui Mamas pia kwa ushirikiano na idara ya turathi za Kenya na shirika la utafiti na kuhifadhi mazingira la Wyss Academy, wanamiliki bustani la mbogamboga za kiasili mfano mchicha, mnavu na viungo kama mchaichai. Hakika, utamaduni na sanaa ni vyanzo muhimu vya kuhifadhi mila na asili ya jamii yoyoye ile na pia kitega uchumi muhimu. 

Shuka maarufu la Maasai utambulisho wa utamaduni

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *