Wengi wanafuatilia England, ambako klabu za ligi ya Premier tayari zimetumia takribani dola milioni 450, Manchester City ikiongoza kwa matumizi ya kumsajili winga Antoine Semenyo na beki Marc Guehi kwa jumla ya dola milioni 115.
Maswali yanaibuka iwapo Liverpool wataongeza nguvu kwenye safu yao ya ulinzi iliyoandamwa na majeraha, huku wakihusishwa na beki chipukizi Jérémy Jacquet wa Rennes.
Crystal Palace nao wanaweza kumuuza mshambuliaji Jean-Philippe Mateta, anayevutiwa na AC Milan, huku Chelsea wakisubiriwa kama watafanya usajili wowote licha ya kuwa na historia ya kuwa na shughuli nyingi sokoni.
Je Athletico itafanikiwa kwa Lookmann
Atletico Madrid wako hatua moja tu kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Nigeria Ademola Lookman kutoka Atalanta, huku klabu hiyo pia ikiripotiwa kumtazama kiungo wa Mexico Obed Vargas wa Seattle Sounders. Atletico tayari wamewauza Conor Gallagher kwenda Tottenham na Giacomo Raspadori kurejea Atalanta.
Katika dirisha hili, Barcelona wamemrejesha beki João Cancelo kwa mkopo kutoka Al-Hilal, huku kipa mkongwe Marc-André Ter Stegen akipelekwa Girona kwa mkopo baada ya kupoteza namba kwa Joan García. Real Madrid wamesalia kimya, wakifanya dili moja tu la kumpeleka mshambuliaji chipukizi Endrick kwa mkopo Lyon.
Atletico walithibitisha Jumapili kuwa Lookman tayari yuko Madrid kwa vipimo vya afya na kukamilisha mkataba wake. Vyombo vya habari vya Uhispania vinaripoti kuwa Atletico watalipa takribani euro milioni 35 kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 28.
Lookman ameng’ara tangu ajiunge na Atalanta mwaka 2022 akitokea RB Leipzig, akifunga mabao 55 katika mashindano yote. Alijizolea umaarufu zaidi kwa kufunga hat-trick kwenye fainali ya Europa League 2024 dhidi ya Bayer Leverkusen, ushindi uliowapa Atalanta taji lao la kwanza la Ulaya na kuvunja rekodi ya mechi 51 bila kupoteza ya Leverkusen. Alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matatu kwenye fainali ya Ulaya tangu 1975.
Mzaliwa wa London, Lookman alianza soka Charlton Athletic kabla ya kujiunga na Everton mwaka 2017. Baada ya kukosa nafasi ya kudumu, alitolewa kwa mkopo RB Leipzig, ambako alifanya vizuri na baadaye kusajiliwa moja kwa moja mwaka 2019. Hata hivyo, nafasi chache Bundesliga zilimfanya atumwe kwa mkopo Fulham na Leicester City kabla ya kuibuka upya Italia na Atalanta.
Sasa, chini ya Diego Simeone, Lookman anatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Atletico Madrid, ambao wako nafasi ya tatu LaLiga wakiwa na pointi 45, pointi 10 nyuma ya vinara Barcelona. Atleti wanatarajia uwezo wake wa kufumania nyavu utawasaidia katika kampeni zao, ikiwemo mchuano wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Club Brugge baadaye mwezi huu.
RB Leipzig wametangaza usajili wa wachezaji wawili Jumatatu: Brajan Gruda, kinda wa Ujerumani kutoka Brighton kwa mkopo, na Ayodele Thomas, winga mwenye umri wa miaka 18 kutoka PSV Eindhoven.