Kulingana na jumuiya ya wanawake, kuelekea uchaguzi mkuu askari wa vyombo vya usalama walilenga kuwatia hofu wanawake wanasiasa hasa wa upinzani wasitekeleze haki zao za kidemokrasia.
Hii imetokana na visa mbalimbali ambapo wanawake wafuasi na wagombea wa upinzani wamehujumiwa waziwazi na kujeruhiwa katika vurugu za kampeni za uchaguzi.
Mwanamke kwa jina Olivia Lutaaya mwenye watoto watatu na mfuasi maarufu wa chama kikuu cha upinzani NUP ambaye alikuwa amezuiliwa gerezani tangu uchaguzi wa mwaka 2021 alikamatwa tena katika kipindi cha kampeni na kufunguliwa mashtaka ambayo wanawake wengi wanaelezea kuwa yalilenga kumkomesha baada ya kupewa msamaha mara ya kwanza na rais Museveni.
Kulingana na wanawake hao, mienendo ya kuwanyanyasa kisiasa imewasababisha wengi kuamua kutoshiriki katika shughuli za uchaguzi kuanzia kupiga kura hadi kugombea.
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi wa uliofanyika mwezoi Januari hapakuwa na mwanamke aliyegombea kiti cha urais kama ilivyokuwa hapo awali na pia angalau asilimia 48 ya wapiga kura hawakushiriki zoezi hilo.
Idadi kubwa ya hawa inaelezewa kuwa wanawake kwani wao pia ndio hujumuisha idadi kubwa ya wapiga kura.
Kuvamiwa kwa mke wa Bobi Wine
Mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uchaguzi, mke wa aliyekuwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alivamiwa nyumbani kwao na askari wa vyombo vya usalama.
Akiwa hospitalini alikopelekwa kupata matibabu Barbie Kyagulanyi alidai kuwa mbali na askari hao kuharibu nyumba yao na pia kupora vitu mbalimbali walimnyanyasa kimwili na kujeruhiwa.
Kisa hicho pamoja na kile cha mwanaharakati wa haki za kidemokrasia Sarah Birete kukamatwa na kuzuiliwa kwa siku kadhaa kabla ya kufikishwa mahakamani alikosomewa mashtaka ya kupatikana na orodha za wapiga kura bila idhini ni baadhi ya vile wanavyotoa mifano wanawake hao kuhusiana na suala zima la dola kujaribu kuwatishia wasijihusishe na siasa.
Mwanaharakati Miria Matembe na Sarah Birete ambaye aliachiwa siku ya Jumatano kwa dhamana wanasema anasema matukio kama hayo yanarudisha nyuma ari ya ushiriki kamilifu wa wanawake katika masuala ya siasa.
Kuzuiliwa kwa wanasiasa wanawake wa NUP
Siku chache kabla ya uchaguzi wanawake viongozi wakuu wawili wa NUP walitekwa kutoka kwenye makaazi yao na hadi sasa hawajulikani waliko.
Vyombo vya usalama na kisheria vimekanusha kuwa waliwakamata Dkt. Lina Zedriga makamu wa rais wa chama cha NUP kanda ya kaskazini na pia Jolly Jackline Tukamushaba wa kanda ya magharibi mwa Uganda.
Hata katika kipindi hiki ambapo shughuli za kuhakiki kura za serikali za mitaa ikiendelea, wanawake kadhaa wa upinzani wamedai kupokonywa ushindi wao.
Badala yake wale wa chama tawala na wanaume waliogombea dhidi yao ndiyo wanatangazwa washindi.
