Kurejea kwa shughuli hizi ni sehemu ya mfumo uliobainishwa kwa umakini. Kufunguliwa huku, ambako kulijumuishwa katika mpango wa Marekani uliowasilishwa Oktoba mwaka jana, ambao  umeainisha mipaka kwa kupitisha wakazi wa eneo la Palestina pekee.

Ingawa hatua hii inaelezwa kuwa chanya, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA linaangazia kuwepo kwa mwenendo unaokinzana.

Linasema kuwa “katika saa 24 zilizopita, Wapalestina 30 wameuawa katika mashambulizi ya anga, licha ya kwamba usitishaji vita umeendelea tangu Oktoba 2025”.

Hali hii ni ukumbusho kwamba hofu na kutokuwa na uhakika bado vinaendelea katika eneo la Palestina.

“Upatikanaji wa misaada bado ni mdogo, masuala ya ulinzi bado yapo, na mahitaji ya kibinadamu bado ni makubwa kutokana na vikwazo vya sasa vya kiutendaji,” amesema Sam Rose, Mkurugenzi wa Masuala wa UNRWA huko Gaza, kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X.

Wagonjwa wakijitayarisha kwa usafirishaji katika Hospitali ya Al-Amal huko Rafah, Gaza, inayoshirikiana na Jumuiya ya Palestina ya Mwezi Mwekundu na inayoungwa mkono na WHO.

WHOinasimamia mchakato wa wagonjwa wanaosafiri kwenda Misri kupata matibabu

Kivuko kitaratibiwa na Misri

Kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA, imefafanua taratibu za kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah.

Kivuko hicho kitaratibiwa kwa kushirikiana na Misri na kusimamiwa na Muungano wa Ulaya, sawa na utaratibu uliowekwa Januari 2025.

Hivyo basi, kurejea Gaza kutoka Misri kutaruhusiwa tu kwa wakazi walioondoka katika Ukanda wa Gaza wakati wa vita, na baada ya kupata kibali cha awali kutoka kwa vyombo vya usalama vya Israel.

Watakaguliwa na Muungano wa Ulaya katika kivuko cha Rafah, kisha kufanyiwa mchakato wa pili wa utambuzi na ukaguzi katika korido maalum inayosimamiwa na jeshi la Israel katika eneo lililo chini ya udhibiti wake.

Wakati huohuo, takwimu zinaonesha kiasi cha misaada ya kibinadamu kinachoingia Gaza. Kati ya Januari 23 na 29, angalau tani 13,800 za misaada ya kibinadamu iliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na washirika wake zilipakuliwa katika vituo vya mipakani vya Gaza.

Takriban asilimia 60 ya shehena hizo zilikuwa ni chakula, pamoja na vifaa vya makazi, vifaa vya shule, bidhaa za afya, mafuta na vifurushi vya lishe.

Kwa jumla, kati ya tangazo la usitishaji vita tarehe 10 Oktoba 2025 na Januari 29, 2026, angalau shehena 272,000 za bidhaa za kibinadamu zilipakuliwa na shehena 270,000 zikakusanywa katika vituo mbalimbali vya mipakani.

“Takriban shehena 1,500, au chini ya asilimia 1 ya misaada iliyowasilishwa, ilizuiwa wakati wa usafirishaji wake ndani ya Gaza,”  shirika la Umoja wa OCHA imesisitiza katika ripoti yake, ikibainisha kuwa takwimu hizi hazijumuishi misaada ya pande mbili wala sekta ya kibiashara.

Wagonjwa, ikiwa ni pamoja na wengine katika viti vya magurudumu, wanatayarishwa kusafirishwa katika Hospitali ya Al-Amal huko Gaza, inayoshirikiana na Jumuiya ya Palestina ya Mwezi Mwekundu.

Wapalestina waliojeruhiwa wakiwa katika viti mwendo wakati wakisubiri kuomba ruhusa ya kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Ukingo wa Magharibi: vita vya kimya visivyoripotiwa 

Wakati macho ya dunia yakiwa bado yameelekezwa Gaza, UNRWA inaeleza kuwa Ukingo wa Magharibi pia unashuhudia ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

UNRWA imesisitiza kuwa katika “vita hivi vya kimya visivyoripotiwa vya kutosha, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel umekuwa ukikumbwa na viwango vya vurugu ambavyo havijawahi kushuhudiwa tangu Oktoba 2023.

Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya Wapalestina 1,000, karibu robo yao wakiwa watoto, wameuawa. Wakati huo huo, mashambulizi ya walowezi wa Israel yanaendelea bila kukoma, na jamii za Kipalestina zinaendelea kutishwa, kuhamishwa na kunyimwa vyanzo vyao vya riziki.

“Adhabu haitolewi. Makumi ya maelfu ya watu bado wameyakimbia makazi yao mwaka mmoja baada ya kuanza kwa Operesheni ukuta wa chuma au Iron Wall ya Israel kumekuwa na ufurushwaji mkubwa zaidi wa watu tangu 1967. Nyumba zao sasa zinabomolewa hatua kwa hatua ili kuwazuia kurejea,” amesema Kamishna Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini, kwenye ukurasa wake wa X.

Mvulana mdogo aliyevaa shati nyekundu anaelekeza gari nyeupe la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa lililopakiwa nje ya Hospitali ya Al-Amal huko Gaza, akiwa na watu na majengo katika mandhari ya nyuma.

Habari za Umoja wa Mataifa

Picha za gari la WHO wakati familia zinawaaga watu wao wanaosafiri kwenda Misri kupata matibabu

Wanawake kunyimwa huduma za afya ya uzazi

Hali hii mbaya inaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake wajawazito na upatikanaji wao wa huduma muhimu. Safari ya kujifungua imekuwa njia iliyojaa vikwazo na hofu.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, vizuizi vya barabarani, vituo vya ukaguzi, amri za kutotoka nje na ukosefu wa usalama mara kwa mara husababisha kucheleweshwa au kuzuiwa kabisa kwa upatikanaji wa huduma muhimu, hali inayowaweka wanawake wajawazito na watoto wachanga katika hatari kubwa.

Changamoto hizi zinaongeza mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya ambao tayari uko dhaifu. Mfumo wa afya unaendelea kuwa chini ya shinikizo kubwa. Ni asilimia 42 pekee ya vituo vya afya katika Ukingo wa Magharibi vinavyofanya kazi kikamilifu, huku wahudumu wa magari ya kubeba wagonjwa na watoa huduma maalum za afya wakikumbwa mara kwa mara na ucheleweshaji, vizuizi, na wakati mwingine mashambulizi ya kimwili.

Hali hii pia inasababisha upatikanaji mdogo wa huduma za afya ya uzazi kwa zaidi ya wanawake 230,000, wakiwemo wanawake wajawazito 4,800, hasa katika majimbo ya Jenin, Tulkarm na Tubas, ambako ukosefu wa usalama na vikwazo vya utembeaji ni vikubwa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *