Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Karim Amri, ameongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kagera kufanya ziara ya kuimarisha chama na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Mutukula, Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera.
Katika ziara hiyo, MNEC Karim Amri ameambatana na Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Ndg. Mollel, pamoja na Katibu wa Miradi wa CCM Mkoa, ambapo kwa pamoja walipata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na chama, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.
Akiwa katika Kata ya Mutukula, MNEC Karim Amri amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mutukula pamoja na jengo la OPD, miradi inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Aidha, amekagua ujenzi wa jengo la Benki ya CRDB Tawi la Mutukula linalojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za kifedha na kukuza uchumi wa wananchi.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, MNEC Karim Amri ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM ya 2025–2030, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni kielelezo cha dhamira ya chama katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Vilevile, amempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Awamu ya Sita wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta na kusimamia utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo katika Mkoa wa Kagera na nchini kwa ujumla.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa chama kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi kupitia Ilani ya 2025–2030 zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
(Feed generated with FetchRSS)