Azimio hilo linataka amani ya kina, ya haki na ya kudumu, pamoja na kubadilishana wafungwa wa vita na kurejeshwa kwa raia waliolazimishwa kuhamishwa, wakiwemo watoto.
Azimio hilo lmepitishwa kwa kura 107 za kuunga mkono, 12 za kupinga na 51 za kujizuia, wakati Baraza Kuu likiendelea na Kikao chake Maalum cha Dharura cha Kumi na Moja (ESS-11).
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lapiga kura na kupitisha azimio kuhusu Ukraine.
Vita ukiukwaji wa wazi wa Chata ya UN
Kupitia hotuba iliyowasilishwa kwa niaba yake, Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock ameeleza kuwa vita hivyo “vilianzishwa na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kwa ukiukwaji wa wazi wa Chata yetu.”
Amekumbusha kuwa miaka minne imepita tangu uvamizi kamili, na takriban miaka 12 tangu kutwaliwa kinyume cha sheria kwa Crimea na Sevastopol, huku mateso ya wananchi wa Ukraine yakiendelea.
“Maelfu ya raia wa Ukraine wameuawa au kujeruhiwa,” amesema, akibainisha kuwa mwaka 2025 umekuwa mbaya zaidi kwa raia tangu vita vianze. Takribani watu milioni nne wamekimbia makazi yao ndani ya nchi, na milioni 5.7 wanaishi kama wakimbizi duniani kote.
“Nyumba, vituo vya afya, shule na hasa mitambo ya umeme na gridi za nishati vimeshambuliwa kwa makusudi na kuharibiwa. Huu ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu,” amesisitiza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Betsa Mariana akitoa hotuba katika kikao maalum cha dharura cha kumi na moja cha Baraza Kuu kuhusu Ukraine.
Dunia Inatazama
Huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikwama kushindwa kuchukua hatua, Baraza Kuu limepitisha maazimio manane tangu kikao hicho maalum kilipoanza mwaka 2022.
“Tangu uvamizi uanze, Baraza Kuu limeendelea kuwa wazi, thabiti na lisilotetereka,” amesema, akiliita chombo hicho “sauti ya maadili ya jumuiya ya kimataifa.”
“Madhara yanazidi mipaka ya Ukraine kuanzia Myanmar hadi Venezuela, Gaza na Sudan,” ameonya. “Dunia inatazama.”
Ukraine yakataa ishara hatari
Kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo, mjumbe wa Ukraine Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Betsa Mariana alipinga mapendekezo ya kufutwa kwa baadhi ya aya muhimu, akiyataja kuwa “yanatia wasiwasi mkubwa na hayawezi kukubalika.” Ameeleza “masikitiko makubwa kuhusu hoja ya kugawanya kura iliyowasilishwa na Marekani”.
“Kudhoofisha au kuondoa lugha hii kungetuma ishara hatari sana kwamba kanuni hizi zinaweza kujadiliwa,” amesema, akitetea marejeo ya Chata ya Umoja wa Mataifa na misingi ya sheria za kimataifa. Ukraine ilipiga kura kupinga hoja hiyo, ikisisitiza kuwa mamlaka na uadilifu wa mipaka haviwezi kuwekewa masharti.
Fikirieni nyuzi joto -20°C bila vipasha joto
Mwakilishi wa Ukraine, Bi. Betsa, ameeleza ukubwa wa mashambulizi ya hivi karibuni, akisema kati ya tarehe 8 na 15 Februari pekee, Moscow ilirusha droni 1,300 za mashambulizi, mabomu ya angani zaidi ya 1,200 na makombora 50, mengi yakiwa ya masafa marefu au balistiki.
Amewataka wajumbe kutafakari hali halisi ya kibinadamu “Fikirieni nyumba zenu hakuna Vipasha joto, hakuna umeme, hakuna maji katika nyuzi joto -20 za Selsiasi. Hivyo ndivyo wakazi wa Kyiv na miji mingine mingi ya Ukraine wanavyoishi majira ya baridi.”
Amesisitiza kuwa ingawa Ukraine iko tayari kwa maelewano magumu, amani lazima iwe “ya heshima, ya haki na ya kina.”
Anna Evstigneeva, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Shirikisho la Urusi, akitoa hotuba katika kikao mahsusi cha dharura cha kumi na moja cha Baraza Kuu kuhusu Ukraine.
Urusi yataka diplomasia
Mwakilishi wa Russia Anna Evstigneeva, ambaye ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Shirikisho la Urusi amezitaka nchi wanachama kuipa kipaumbele diplomasia badala ya matamko.
“Leo, wakati dirisha halisi la fursa limefunguka kwa suluhu ya kisiasa ya mgogoro wa Ukraine, tunachopaswa kuzungumzia kwanza si matamko, bali diplomasia,” amesema, akirejelea mazungumzo yanayoendelea Abu Dhabi na Geneva.
“Huu ni wakati wa kujizuia kwa busara na kuheshimu mchakato wa mazungumzo,” ameongeza, akisema ikiwa lengo la kweli ni amani, “vitendo lazima viendane na maneno, si kupingana.”