Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu jijini New York, Marekani na Geneva, Uswisi, tarehe 23 Februari imemnukuu Guterres akisema uvamizi huo ulifanyika “kwa kukiuka Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.” 

Vita hivi ni doa la dhamira ya kibinadamu

Amesema vita vinavyoendelea ni  “doa katika dhamira yetu ya pamoja” na kuonya kuwa vinaendelea kuwa tishio kubwa kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.

“Kadiri vita vinavyoendelea, ndivyo vinavyozidi kuongeza vifo,” amesema Guterres akisisitiza kuwa hadi sasa vita hivyo vimesababisha madhara makubwa kwa raia, akibainisha kuwa mwaka 2025 ulishuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo vya raia nchini Ukraine tangu kuanza kwa mzozo huo.

Wazima moto huko Kyiv, Ukraine, wanapambana na moto katika jengo la viwanda lililoharibiwa sana wakati wa hali ya baridi kali. Barafu inafunika muundo na eneo linalozunguka wakati wafanyakazi wanafanya kazi kudhibiti moto na kuzuia kuenea zaidi.

© UNICEF/Ian Dobronosov

Wazima moto wanapambana kuzima moto katika jengo la viwanda lililoharibiwa huko Kyiv, Ukraine.

Raia ndio wanalipa gharama kubwa

“Raia ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa mzozo huu,” amesema Katibu Mkuu, akielezea ongezeko la vifo kuwa “halikubaliki kabisa.”

Katibu Mkuu amerejelea wito wake wa “kusitishwa mara moja, kikamilifu na bila masharti kwa mapigano” kama hatua muhimu ya kwanza kuelekea kufikiwa kwa amani ya haki, ya kudumu na jumuishi. 

Makubaliano ya amani yazingatie Chata ya UN

Amesisitiza kuwa makubaliano yoyote ya amani lazima yaendane na misingi ya Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, pamoja na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.

“Ili amani iwe ya haki, lazima izingatie Chata ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na iheshimu uhuru, mamlaka kamili na uadilifu wa mipaka ya Ukraine,” amesema Guterres.

Msimamo wa UN katika mustakabali wa amani Ukraine

Vita vilianza tarehe 24 Februari 2022, wakati majeshi ya Urusi yalipoanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi katika maeneo mbalimbali ya Ukraine. 

Tangu wakati huo, maelfu ya raia wameuawa, mamilioni wamekimbia makazi yao, na miundombinu muhimu kuharibiwa vibaya.

Akithibitisha tena jukumu la Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi za kidiplomasia, Guterres amesema “Umoja wa Mataifa uko tayari kuchangia katika juhudi zote” zinazolenga kumaliza mzozo huo na kufikia amani endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *