
Kikao hicho kilianza jana ambapo ICC inasema ni hatua muhimu itakayoamua kama kesi hiyo itaendelea hadi kusikilizwa rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa ya ICC, madhumuni ya kikao hicho cha siku nne kinachofanyika The Hague ni kubaini kama kuna “misingi thabiti ya kuamini” kwamba Duterte alitenda makosa kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa ICC.
“Wakati wa kikao hiki, Mahakama haitatoa uamuzi wowote iwapo Duterte ana hatia au la,” amesema Jaji Kiongozi, Iulia Antoanella Motoc kutoka Romania.
Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 80 pia aliwahi kuwa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Davao – mojawapo ya majiji makubwa nchini Ufilipino.
Anashukiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu wa mauaji na jaribio la mauaji yanayodaiwa kutendwa kati ya tarehe 1 Novemba 2011 na 16 Machi 2019.
Mashtaka na kukamatwa
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kesi hiyo inajumuisha makosa matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu: mauaji ndani au karibu na Jiji la Davao wakati wa kipindi chake cha umeya yanayodaiwa kufanywa na kundi linaloitwa “Kikosi cha Mauaji cha Davao”; na wakati wa urais, mauaji ya wanaoitwa “walengwa wa kiwango cha juu”; na mauaji pamoja na majaribio ya mauaji katika operesheni za usafishaji wa kitongoji.
“Duterte na washirika wake walikuwa na mpango wa pamoja wa kuwadhibiti wanaodaiwa kuwa wahalifu nchini Ufilipino…kupitia uhalifu wa kikatili, ikiwemo mauaji,” amesema afisa wa mahakama wakati akisoma mashtaka ya upande wa mashtaka.
Hati ya kukamatwa ilitolewa kwa siri tarehe 7 Machi 2025 na kuainishwa upya siku nne baadaye. Tarehe 12 Machi, Duterte alikabidhiwa mahakamani baada ya kukamatwa na mamlaka za Ufilipino.
Kwa sasa anazuiliwa katika Kituo cha Kizuizini cha ICC kilichopo Scheveningen, nchini Uholanzi.
Jukumu la uthibitisho
Washukiwa katika ICC huchukuliwa kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo pasipo shaka ya msingi.
“Jukumu la uthibitisho ni la Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC, ambayo lazima itoe ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka dhidi ya Duterte kwa kiwango kinachohitajika cha uthibitisho,” amesema Jaji Motoc.
Ushiriki wa manusura
Katika kikao hicho, waendesha mashtaka – wakiongozwa na Naibu Mwendesha Mashtaka Mame Mandiaye Niang pamoja na mawakili waandamizi wa kesi – wanapaswa kuunga mkono kila shtaka kwa ushahidi wa kutosha. Timu ya utetezi ya Duterte – inayoongozwa na Nicholas Kaufman – pia itawasilisha hoja zake.
Wawakilishi wa kisheria wa waathiriwa 539 watawasilisha hoja zao mbele ya majaji.
Hatua zinazofuata
Ndani ya siku 60 za kalenda baada ya kikao hiki cha siku nne kumalizika, majaji watatoa uamuzi wa maandishi kuhusu kama kesi itaendelea.
Wanaweza kuthibitisha baadhi au mashtaka yote na kuipeleka kesi hiyo kwenye chumba cha kusikiliza kesi; kukataa kuthibitisha mashtaka na kusitisha mashauri; au kuahirisha kikao na kuomba ushahidi wa ziada au marekebisho.
Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya Uhalifu
ICC ni mahakama ya kudumu ya kimataifa yenye makao yake The Hague inayowafungulia mashtaka watu binafsi wanaotuhumiwa kwa makosa mazito zaidi chini ya sheria za kimataifa, ikiwemo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na uhalifu wa uchokozi.
Ilianzishwa kwa Mkataba wa Roma, mkataba uliopitishwa mwaka 1998 na kuanza kutumika mwaka 2002, unaobainisha mamlaka, nguvu na taratibu za Mahakama hiyo na kuziwajibisha nchi zilizouridhia.