
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi leo Jumanne, Annalena Baerbock, ambaye ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, amesema kuwa miaka minne iliyopita watu barani Ulaya “waliamka katika dunia nyingine kwa sababu vizazi kama changu vimekuwa na fursa ya kuishi maisha ya amani.”
Akiitaka jumuiya ya kimataifa “kufanya kazi kila siku kwa ajili ya amani,” Bi. Baerbock amesisitiza tena umuhimu wa “kusitisha haraka mapigano, tena kwa ukamilifu na bila masharti.”
“Vita hivi lazima hatimaye vikome… Mkataba wowote wa amani lazima uzingatie Chata ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza Kuu,” amesema, akisisitiza kuwa hilo linamaanisha kuheshimu mamlaka, uadilifu wa mipaka na uhuru wa Ukraine.
Baraza Kuu kujadili Ukraine na kupitisha azimio
Maoni ya Bi. Baerbock yametolewa kabla ya kikao maalum cha dharura cha Baraza Kuu kinachotarajiwa kufanyika New York baadaye leo Jumanne, ambapo nchi zinatarajiwa kuchukua hatua kuhusu rasimu ya azimio linalotaka usitishaji mapigano, amani ya haki na ya kudumu kwa mujibu wa sheria za kimataifa, pamoja na hatua kadhaa za kujenga imani kama vile kubadilishana kikamilifu wafungwa wa vita, kuachiliwa kwa watu wote waliowekwa kizuizini kinyume cha sheria na kurejeshwa kwa wote waliowekewa vizuizi na raia waliolazimishwa kuhamishwa na kupelekwa nje ya nchi, wakiwemo watoto.
OCHA kutoka Kyiv
Akizungumza kutoka Kyiv, Mratibu Mkazi na wa Misaada ya Kibinadamu wa UN nchini Ukraine, Matthias Schmale, amesema kuwa 2025 ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa raia tangu kuanza kwa uvamizi kamili mwaka 2022, huku takribani raia 2,500 wakiuawa na zaidi ya 12,000 wakijeruhiwa mwaka uliopita — ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na 2024.
Baadhi ya majengo Kyiv hayakaliki msimu huu wa baridi kali
Amesisitiza athari mbaya za mashambulizi ya kimfumo dhidi ya miundombinu ya nishati yaliyokatiza huduma za umeme, joto na maji kote nchini, na wakati mwingine kuacha miji mizima bila umeme na maji kwa wiki kadhaa.
“Ninaambiwa kuwa Kyiv kuna zaidi ya majengo 3,000 ya ghorofa nyingi ambayo sasa hayafai kukaliwa kwa kipindi chote cha majira ya baridi, hali inayowaweka katika hatari kubwa watu walio katika mazingira magumu zaidi, wazee, watu wenye ulemavu wa kutembea au matatizo ya kiafya, pamoja na familia zenye watoto,” amesema Schmale.
“Matumizi haya ya nishati kama silaha lazima yakome,” amesisitiza.
Vita imefurusha mamilioni ya raia wa Ukraine- UNHCR
Philippe Leclerc, Mkurugenzi wa Kanda ya Ulaya na Mratibu wa Kikanda wa Wakimbizi wa Ukraine katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) amesema kuwa kutokana na vita vinavyoendelea, wakimbizi milioni 5.9 bado wako nje ya Ukraine na milioni 5.7 wako barani Ulaya.
Amesema kuwa uhamishaji wa watu unaendelea, na idadi ya watu waliolazimika kuhamishwa kutoka maeneo yaliyo karibu na uwanja wa mapambano “imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miezi sita iliyopita kutokana na shinikizo la mashambulizi ya kijeshi pamoja na majira haya ya baridi kali.”
Leclerc amesema kuwa licha ya mshikamano mkubwa unaoendelea kuoneshwa kwa waukraine na nchi za Muungano wa Ulaya kwa kutoa hifadhi ya muda, “waukraine wanatazama mustakabali, ujenzi upya wa taifa lao, wa jimbo la Oblast , wa uchumi wao, na kwa hilo watawahitaji wakimbizi.”
Zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi waliohojiwa na UNHCR wanapanga kurejea nyumbani, amesema afisa huyo, licha ya miaka minne ya vita na hali ya kutokuwa na uhakika inayoendelea.
Changamoto za ujenzi mpya
Akizungumzia changamoto za mchakato wa ujenzi upya na uokoaji, Schmale amesema kuna hadi wanajeshi wastaafu milioni moja wanaohitaji kurejeshwa katika jamii ya Ukraine, wengi wao wakiwa na majeraha ya kudumu maishani, ikiwemo kukatwa viungo.
Amesisitiza pia kuwa Ukraine ni “miongoni mwa nchi duniani zilizo na kiwango kikubwa cha mabomu yaliyotegwa ardhini ,” huku karibu robo ya eneo lake likikadiriwa kuwa limeathiriwa na mabomu ya ardhini.
Ujenzi mpya uzingatie misingi ya jamii
Akirejelea “ripoti ya haraka ya tathmini ya uharibifu na mahitaji” iliyozinduliwa Jumatatu na UN kwa kushirikiana na serikali ya Ukraine, Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya, Schmale amesema kuwa gharama zinazokadiriwa za uokoaji ni “dola bilioni 590 katika kipindi cha miaka 10, sawa na mara tatu ya pato la taifa (GDP) la Ukraine mwaka uliopita.”
Aina hii ya ripoti, amesema, haiwezi kikamilifu kuonesha “uharibifu wa maisha ya binadamu, nafsi zao na ustawi wao wa kiakili.”
“Uokoaji lazima uzingatie utu wa binadamu na ujengwe juu ya misingi ya jamii,” amesisitiza.