Hiyo ni kauli ya Jonathan Crickx, Mkuu wa Mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, huko Palestina aliyoitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi kutokea mjini Yerusalemu.
Crickx akiwasilisha matokeo ya mpango wa “The Gaza We Want,” au Gaza Tuitakayo uliozinduliwa na UNICEF ili kukusanya maoni ya watoto kuhusu mustakabali wa Gaza baada ya miaka miwili ya vita, amesema ingawa mateso yanayokabili watoto yamekuwa yakiripotiwa kwa kina, sauti zao zimekuwa hazisikiki vya kutosha katika mipango ya uokoaji na ujenzi upya.
Picha iliyochorwa na watoto wa Gaza kama sehemu ya mpango wa “Gaza We Want” uliozinduliwa na UNICEF mwezi Februari.
Ukusanyaji wa sauti za watoto
Kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, watoto 1,603 wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 18 kutoka majimbo yote matano ya Gaza, wakiwemo watoto wenye ulemavu, walijaza dodoso maalum.
Zaidi ya watoto 11,000 walishiriki kupitia michoro, mashairi, hadithi fupi, barua, michoro ya ukutani na maigizo shughuli zote zikiwa za hiari na salama, bila kumlazimisha mtoto yeyote kukumbuka matukio ya vurugu.
Crickx amesema michoro na kazi za ubunifu si ishara tu bali ni ushahidi, akibainisha kuwa watoto wengi, bila kushirikiana, walichora vitu vinavyofanana: miti, shule, hospitali, barabara safi na viwanja vya michezo ishara ya wazi ya kutaka kurejeshewa utoto wao.
Simulizi za watoto aliokutana nao
Wiki tatu zilizopita huko Deir El Balah, alikutana na Hala, msichana mwenye umri wa miaka 15 katika Kituo cha Kujifunzia cha Muda cha UNICEF, ambaye alisema ndoto yake ni kuwa na nyumba salama, chumba chake binafsi na shule nzuri.
Kwa mujibu wa Crickx, ujumbe huu umejirudia mara nyingi: watoto wanataka makazi bora, usalama na kurejea shuleni.
Picha iliyochorwa na watoto wa Gaza kama sehemu ya mpango wa “Gaza We Want” uliozinduliwa na UNICEF mwezi Februari.
Afisa huyo wa UNICEF amesema tangu kuanza kwa usitishaji mapigano, zaidi ya watoto 135 wameripotiwa kuuawa Gaza, akisisitiza kuwa matakwa ya watoto si ya anasa bali ni misingi ya utoto.
Ujenzi mpya watoto wanataka nini?
Watoto wamependekeza vipaumbele vya wazi kwa mchakato wa ujenzi upya: kwanza usalama, makazi ya dharura, maeneo ya kujifunzia na huduma ya kwanza ya kisaikolojia; kisha nyumba za kudumu, shule, bustani na kliniki; na baadaye Vyuo Vikuu, viwanda na vituo vya kitamaduni.
Crickx amesisitiza kuwa shule zinapaswa kuwa majengo salama yenye madarasa, maji safi, vyoo na viwanja vya michezo si mahema au makazi ya muda kwa waliokimbia makazi yao. Pia ameeleza kuwa watoto wanahitaji hospitali tulivu na salama, pamoja na msaada wa afya ya akili, akibainisha kuwa majeraha ya kisaikolojia hayaishi mara tu mabomu yanapokoma.
Akinukuu maneno ya Mayar, msichana mwenye umri wa miaka 14 aliyejeruhiwa vitani, Crickx amesema watoto wanataka “Gaza nzuri yenye hospitali, shule na majengo salama.”
Ametamatisha kwa kutoa wito kwa watoa maamuzi kuhakikisha kuwa sauti za watoto zinakuwa kiini cha mipango ya uokoaji. “Kusikiliza watoto si hiari,” amesema. “Ni kiwango cha chini kabisa cha ujenzi upya wenye uaminifu.”